
London, England
Pamoja na ubora wa kiungo wa Man United, Paul Pogba, kocha wa muda wa timu hiyo, Ralf Rangnick amesema hatomshawishi mchezaji huyo abaki katika klabu hiyo kama ana mawazo ya kuondoka.
Mkataba wa sasa wa Pogba na Man United unafikia ukomo mwakani majira ya kiangazi na hadi Januari mwakani atakuwa huru kuanza mazungumzo na klabu nyingine kama ataona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Akifafanua kuhusu uamuzi wake kwa mchezaji huyo Rangnick alisema, “Siwezi kusema hana sifa za kuendelea kubaki hapa lakini wachezaji wanatakiwa wawe wanataka kubaki na kuichezea klabu.”
Rangnick alisema kama mchezaji hataki kuichezea klabu kubwa yenye mashabiki wengi ya Man United hata kwa mkataba mrefu hadhani kama kuna maana kumshawishi ili abadili mawazo yake.
Pogba ambaye mwaka 2018 alikuwamo katika kikosi cha Ufaransa kilichotwaa taji la dunia inadaiwa kuwa huduma yake inahitajika katika klabu kadhaa kubwa barani Ulaya.