
Sao Paulo, Brazil
Nyota wa soka wa zamani wa Brazil aliyetwaa taji la Dunia mara tatu, Pele amerudishwa hospitali hali ambayo imemgusa nyota wa Man United, Cristiano Ronaldo ambaye amemtumia ujumbe wa kumfariji.
Mapema wiki hii, Pele alirudishwa katika Hospitali ya Albert Einstein Hospital mjini Sao Paulo kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye utumbo mpana.
Kutokana na hali hiyo, Ronaldo amemtumia ujumbe Pele mwenye umri wa miaka 81 wa kumtakia heri apone haraka.
Pele aligundulika kuwa na uvimbe kwenye utumbo, Agosti mwaka huu wakati akiwa katika utaratibu wake wa kawaida wa kwenda hospitali kuangaliwa afya na hivyo mwezi mmoja baadaye akafanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo.
Awali Pele alituma ujumbe wenye utani kupitia Instagram mara baada ya kufanyiwa upasuaji na kupata nafuu pale aliposema kwamba anajiandaa kurudi tena uwanjani.
Mbali na Ronaldo, Pele ametumiwa ujumbe na mamia ya watu wakiwamo mashabiki wake duniani kote wakimtakia afya njema huku wakionyesha kuguswa na afya yake naye akawajibu akiwaambia kwamba wasiwe na wasiwasi kwani anajiandaa kwa ajili ya msimu wa sikukuu.
“Marafiki zangu tangu Septemba 30 nilipotoka hospitali mnafahamu kwamba nilifanyiwa upasuaji mdogo ambao ni sehemu ya matibabu, leo niko Hospitali ya Albert Einstein nikifanyiwa matibabu ya mwisho kwa mwaka 2021, nataka kuwaeleza nyinyi mafanikio haya. Yote kwa yote kila ushindi mdogo unatosha kuwa sababu ya kusherehekea, au siyo?”
