Na mwandishi
Yanga imepanda hadi nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Coastal Union ya Tanga bao 1-0 mechi iliyochezwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Bao hilo pekee la Yanga lilipatikana dakika ya 24 mfungaji akiwa ni Jean Baleke ambaye hilo ni bao lake la kwanza katika ligi kuu msimu huu tangu ajiunge na timu hiyo.
Baleke alifunga bao hilo kutokana na mpira wa kona iliyochongwa na Maxi Nzengeli na kuokolewa vibaya na Haroub Mohamed kabla ya kumkuta Khalid Aucho aliyemsogezea Baleke na kuujaza wavuni.
Coastal licha ya kufungwa bao hilo walilichachafya mara kadhaa lango la Yanga ambalo katika mechi ya leo lililindwa vyema na kipa namba mbili Aboubakar Khomeini.
Kwa upande wa Coastal kipa wao Chuma Mgeni naye hakuwa nyuma katika kudhibiti mashambulizi ya mara kwa mara ya Yanga na haikushangaza hadi dakika 90 zinamalizika Yanga walipata bao moja tu.
Coastal nusura wasawazishe bao baada ya Ernest Malongo kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu dakika chache kabla ya kutimia dakika 90 lakini wakati akiupiga mpira huo alikuwa tayari ameotea.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 21 katika mechi saba ikiwa haijapoteza hata mechi moja na kutua nafasi ya pili iliyokuwa ikishikiliwa na mahasimu wao, Simba huku Singida BS wakiendelea kushikilia usukani.
Baada ya kuona mambo hayaendi kama ilivyotarajiwa, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa akiwatoa Baleke, Maxi Nzengeli na Aziz Ki na nafasi zao kuingia Pacome Zouzoua, Clatous Chama na Prince Dube.
Mabadiliko hayo bado hayakubadili matokeo hata pale alipomtoa Yao Kouasi aliyeumia na nafasi yake kuingia Duke Abuya na Clement Mzize ambaye nafasi yake aliingia Aziz Andambwile lakini matokeo yalibaki 1-0.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, KMC ikiwa ugenini iliilaza Tanzania Prisons mabao 2-1, mabao ya washindi yakifungwa na Daruwesh Saiboko dakika za 16 na 60 wakati bao la Prisons lilifungwa na Oscar Mwajanga dakika ya 74.
Soka Yanga yaibutua Coastal 1-0
Yanga yaibutua Coastal 1-0
Read also
