Na mwandishi wetu
Simba imetoa kichapo cha mabao 3-0 kwa Namungo katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Kinondoni jijini Dar es Salaam Ijumaa hii jioni Oktoba 25, 2024.
Beki Shomari Kapombe alikuwa wa kwanza kuandika bao la Simba dakika ya tano, bao lililotokana na juhudi za beki huyo aliyecheza kwa kiwango cha juu akipanda mbele mara kwa mara kusaidia mashambulizi ya timu yake.
Dakika takriban 30 baadaye, Simba iliandika bao la pili lililofungwa na kiungo Jean Ahou aliyeingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Awesu Awesu ambaye aliumia.
Karamu ya mabao ya Simba ilikamilishwa na Debora Fernandes Mavambo zikiwa zimebakia dakika tano kabla ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo.
Kwa ushindi huo Simba sasa wamefikisha pointi 19 katika ligi hiyo wakiwa tayari wamecheza mechi nane, wameshinda sita, wamepoteza moja na kutoka sare moja wakishika nafasi ya pili.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa siku hiyo hiyo, Azam FC wakiwa nyumbani Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam waliibugiza Ken Gold mabao 4-1.

Mabao ya washindi yalifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa penalti katika dakika ya 20 akifuatiwa na Jhonier Blanco aliyeandika bao la pili dakika ya 37 na kuwafanya Azam waende mapumziko wakiwa mbele kwa 2-0.
Kasi ya Azam iliendelea kipindi cha pili kwa bao la tatu lililofungwa na Gibril Sillah dakika ya 50 na la nne likifungwa na Cheikh Sidibe dakika ya 72 wakati bao pekee la Ken Gold lilifungwa kwa penalti na Joshua Ibrahim dakika ya 87.
Kwa ushindi huo, Azam sasa imefikisha pointi 18 katika mechi tisa ikiwa nafasi ya nne na hadi sasa imepoteza mechi moja na kutoka sare mara tatu.
Nao vinara wa ligi hiyo, Singida BS wakiwa nyumbani walifanikiwa kuichapa Fountain Gate mabao 2-0 huku mabao ya washindi yakifungwa na Josephat Daba dakika ya 54 na Ayoub Lyanga dakika 10 baadaye.
Kwa ushindi huo, Singida BS wameendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa wamefikisha pointi 22 katika mechi nane, hawajapoteza hata mechi moja, wana sare moja.
Ligi hiyo itaendelea Jumamosi Oktoba 26, 2024 ambapo Prisons ya Mbeya watakuwa wenyeji KMC, Yanga watakuwa wageni wa Coastal Union na Dodoma Jiji wataikaribisha JKT Tanzania.