Moscow, Urusi
Rufaa iliyokatwa na Shirikisho la Soka la Urusi (FUR) na klabu za soka nchini humo kupinga kufungiwa kushiri michuano ya soka barani Ulaya na duniani kwa ujumla imekataliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS).
Klabu za soka nchini Urusi na timu ya Taifa kwa pamoja zimepigwa marufuku kushiriki mashindano yote yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) baada ya nchi hiyo kuivamia Ukraine.
Kutokana na uamuzi huo, Urusi iliamua kukata rufaa sita ambazo zote zimegonga mwamba mbele ya CAS baada ya kusikilizwa na mahakama hiyo kati ya Julai 5 na 11 mwaka huu.
“Timu ya CAS iliyokaa ilizingatia maslahi mapana ya soka na ukubwa wa mgogoro kati ya Urusi na Ukraine pamoja na umma na serikali duniani kote zilivyolichukulia tukio la uvamizi huo na kuleta hali tete hadi Fifa na Uefa wakalazimika kuchukua hatua dhidi ya Urusi,” ilieleza taarifa ya CAS.
Aprili mwaka huu, Urusi walikata rufaa CAS mara baada ya nchi hiyo kufutiwa na Fifa ushiriki wao wa kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar, Novemba mwaka huu.
Wakati FUR wakiwa wamekata rufaa dhidi ya Fifa na Uefa, klabu za Sochi, Dynamo Moscow, CSKA Moscow, Zenit St Petersburg na SKA Moscow zilikata rufaa dhidi ya Uefa.
Kimataifa Rufaa ya Urusi yakwama CAS
Rufaa ya Urusi yakwama CAS
Related posts
Read also