Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amempongeza kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Pacome Zouzoua kwa kiwango bora anachokionesha kwenye michuano yote ambayo timu hiyo inashiriki ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gamondi alisema pamoja na ubora na kiwango alichokuwa nacho mchezaji huyo lakini anapaswa kuongeza ubunifu na umakini ili kufanya mambo yake kwa usahihi zaidi.
“Pacome ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana na amekuwa akijitoa, nafurahi kuona hilo lakini hapaswi kuridhika na anapaswa kuongeza umakini na kufanya mambo kwa usahihi zaidi,” alisema Gamondi.
Alisema anaamini Pacome ana vitu vingi bado hajavionesha lakini kitu cha msingi kwake anapaswa kucheza kwa kufuata mfumo wa timu kama anavyofanya sasa na kushirikiana kwa karibu na wachezaji wenzake.
Gamondi alisema anaridhishwa na viwango vinavyooneshwa na wachezaji wengi walio ndani ya kikosi chake lakini Pacome ameonesha utofauti mkubwa hasa katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pacome alijiunga na Yanga msimu huu na tayari ameifungia timu hiyo mabao sita kwenye mashindano yote, kwenye Ligi Kuu NBC amefunga mabao manne na Ligi ya Mabingwa amefunga mawili.
Katika mabao yake mawili ya Ligi ya Mabingwa, yote yaliinusuru Yanga kutopoteza pointi baada ya kufunga kwenye mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Medeama na Al Ahly iliyoisha 1-1 pia.