Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo akisema bado wana nafasi ya kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika watakapoenda kusaka pointi tatu dhidi ya Wydad AC ya Morocco.
“Nawaomba radhi mashabiki wetu, tusahau matokeo yaliyopita ambayo kocha wetu (Abdelhak Benchikha) ameyafanyia kazi mapungufu yaliyopita na sasa nguvu na akili zetu tumezielekeza kusaka ushindi dhidi ya Wydad,” alisema Baleke.
Simba wako Kundi B wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi mbili baada ya kushuka uwanjani mara mbili. ASEC Mimosas ndio kinara ikiwa imejikusanyia pointi nne sawa na Jwaneng Galaxy inayoshika nafasi ya pili na Wydad inaburuza mkia bila.ya pointi.
Baleke alisema anawaomba mashabiki wa Simba kusahau matokeo ya nyuma na kuwataka kuungana kuwa nguvu moja kuelekea kwenye mechi hiyo muhimu ya kutafuta pointi tatu ugenini.
Kuhusu tetesi za kurejea kwenye klabu yake ya TP Mazembe, Baleke alisema bado yupo Simba na anachokifikiria zaidi ni kuona timu yake ikifanikiwa kuvuka katika hatua ya makundi na kwenda robo na hatimaye nusu fainali.