Na Hassan Kingu
Simba SC imetupwa nje ya michuano ya African Football League na Al Ahly ya Misri kwenye hatua ya robo fainali lakini imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kushiriki michuano hiyo mipya Afrika.
Lakini pia imekuwa miongoni mwa timu nane pekee za Afrika zilizoingia kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) chini ya mwamvuli wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Licha ya kuwa timu ya kwanza kung’oka lakini imepongezwa mno kwa mchezo mzuri iliouonesha dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino aliyehudhuria mechi ya kwanza, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2, alielezea alivyoridhishwa na kiwango cha ushindani wa mechi hiyo.
Matokeo ya sare ya 1-1 pale Cairo, Misri pia yaliteka hisia za wengi kwa namna Simba ilivyojitahidi kupambana na kupata sare ya jumla ya mabao 3-3, lakini sheria ya bao la ugenini iliwaondoa kwenye kinyang’anyiro.
Wekundu hao wamezikumbatia sifa hizo, nyuma yake kukiwa na akili ya kocha wao Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye alitumia falsafa na mbinu nyingi kuhakikisha wanapenya hatua inayofuata au hawatoki kwenye michuano hiyo kwa aibu.
Ndio, Afrika Mashariki iliwakilishwa na Simba pekee, hivyo ilibeba mioyo ya nchi zote za Ukanda wa Cecafa na Robertinho alisimamia vyema hilo lakini kanuni na matokeo halisi ya soka yaliikataa Simba.
Hii si mara ya kwanza, Robertinho anaiongoza Simba kupigana kiume hasa katika mechi ngumu kama hizi za mabingwa wa Afrika.
Msimu uliopita Lunyasi walitolewa kwa penalti 4-3 na waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Wydad AC ya Morocco. Hiyo ni baada ya kila timu kushinda bao 1-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Inafahamika ‘matuta’ hayana mwenyewe na kwa mara nyingine timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo haikuwa na bahati upande huo lakini bado hiyo haikufuta ubabe na ‘ubishi’ wa Robertinho kwenye mechi ngumu.
Ukiachana na Simba kukutana na vigingi michuano ya klabu Afrika, ilipokutana na mtani wake, Yanga ambayo iko vizuri na imetawala soka la Tanzania kwa misimu miwili mfululizo, ikizoa makombe ya ndani, Robertinho aliisimamisha kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita na kuichelewesha kutangaza ubingwa wake.
Mwanzoni mwa msimu huu aliinyoa Yanga kwa penalti 3-1, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kutwaa Ngao ya Jamii iliyokuwa ikishikiliwa na Yanga.
Yote hayo ameyafanya ndani ya miezi 10 pekee aliyodumu Simba mpaka sasa akitokea Vipers ya Uganda!
Wakati hayo yakitokea, Robertinho amekuwa hana ‘amani’, anasumbuliwa mno na wakosoaji wa falsafa zake.
Wengine wakiwa ni mashabiki wa Simba ambao mara kadhaa wameshindwa kuwa na hoja zenye nguvu juu ya ukosoaji huo.
Ni kama vile hazungumziwi kabisa kwenye ubora, anaonekana si tishio lakini ndio kocha ambaye ana matokeo ya ushindi wa asilimia 100 kwenye ligi. Ameshinda mechi zote tano.

Timu ya Arsenal ya England ilipewa jina la ‘The Invincibles’ ikiwa na maana ya wasiozuilika baada ya kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo msimu wa 2003-04 bila ya kupoteza mchezo.
Sasa kwa upande wa Robertinho ambaye ana viashiria vya ‘u-invincible’ tangu kuanza kwa msimu huu kwenye ligi, yeye ni kama vile amekuwa ‘invisible’ yaani asiyeonekana kwenye mazuri kutokana na wingu kubwa la ukosoaji lililotanda mbele yake. Haongelewi kwa mazuri lakini amekuwa akiwajibu wanaomkosoa kwa vitendo ndani ya dakika 90 uwanjani.
Miongoni mwa vipenzi vya Robertinho pale Simba ni kiungo wa pembeni, Kibu Denis. Na inafahamika kilichopo kwa baadhi ya mashabiki wa Simba kwa Robertinho ndicho kilichopo kwa Kibu.
Soka la Kibu linaonekana la nguvu nyingi, maarifa kidogo lakini ni kiungo muhimu wa Robertinho katika kikosi chake. Kibu anafanya kwa asilimia kubwa yale anayoelekezwa, anakaa kwenye mfumo unavyotaka.
Anahaha mno uwanjani timu ikiwa haina mpira na anapambana kwelikweli kuwavuruga wapinzani anapokuwa na ‘mali’.
Kibu ndiye aliyepiga shuti la ‘mwana ukome’ la umbali mrefu na kutinga wavuni na kunogesha ushindi wa Simba walipoikunyuga Yanga mabao 2-0.
Ndiye yeye aliyejitwisha ‘kichwa cha kuogelea’ na kuusukuma mpira wavuni akichomoa bao la kwanza katika sare ya 2-2 na Al Ahly.
Yote hayo ni invincible. Robertinho haonekani kwenye mafanikio hayo. Ni tofauti na walivyoimbwa na kuzungumzwa makocha Didier Gomes au Patrick Aussems ‘Uchebe’ waliowahi kuinoa Simba hivi karibuni.
Pengine ujuaji mwingi wa soka wa Watanzania bila ya maarifa stahiki ya mchezo huo katika siku za usoni, yamepelekea yote haya.
Au pengine kufananishwa Simba na Yanga kiuchezaji kila kukicha ndiko kunakopelekea haya na kusahau kuwa hata wababe wa soka Hispania, Real Madrid na Barcelona au wababe wa Misri, Ahly na Zamalek hawafanani uwanjani, kila mmoja ana njia zake na wachezaji wake.
Robertinho, mzee wa ‘objective football’ ana kitu lakini bado hakionekani, pengine hakitaonekana mpaka akiwapa ubingwa ambao Simba hawajawahi kuwa nao, na kuanza kuuthamini mchango wake au atakapoondoka na falsafa zake na timu kuanza kutumia muda mrefu kujengeka tena.
Lakini angalau uongozi wa Simba kwa nyakati tofauti umetoka mbele na kueleza kuunga mkono kila linalofanywa na kocha huyo.
Na kauli hizo ndio uzi pekee unaomshikilia ‘The Invisible Robertinho’ kuendelea kutufundisha upande wa pili wa soka la kisasa lisiloonekana na macho ya wengi.