Zurich, Switzerland
Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter amepinga uamuzi wa Fifa kuruhusu fainali za Kombe la Dunia kuchezwa katika nchi sita za mabara matatu tofauti.
Fifa imezitangaza nchi za Morocco, Hispania na Ureno kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2030 wakati nchi za Marekani Kusini za Uruguay, Argentina na Paraguay zimepewa uenyeji wa mechi tatu ambazo ni maalum kwa kumbikizi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa fainali hizo.
Uamuzi huo umepingwa na Blatter ambaye alikuwa rais wa Fifa kuanzia mwaka 1998 hadi 2015 alipolazimishwa kujiuzulu baada ya uchunguzi kufanywa dhidi yake kuhusu tuhuma za rushwa zilizokuwa zikimkabili.
“Ni jambo la ajabu kugawa fainali hizi, fainali za Kombe la Dunia ni tukio moja, ni muhimu kwa utambulisho wa tukio lenyewe na mipango kwa wageni,” alisema Blatter katika mazungumzo yake na gazeti moja la Switzerland.
Blatter mwenye umri wa miaka 87 sasa, alisema kwamba fainali za Kombe la Dunia 2030 zilipaswa kufanyika Marekani ya Kusini kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 100 ya fainali hizo ambazo zilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Uruguay.
“Kwa sababu za kihistoria, fainali za Kombe la Dunia 2030 zilitakiwa kuwa maalum kwa ajili ya Marekani ya Kusini,” alisema Blatter.
Hii ni mara ya pili kwa Blatter kuipinga Fifa tangu atolewe madarakani, awali alipinga uamuzi wa Fifa kuipa Qatar uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa madai kwamba nchi hiyo ni ndogo mno.