Na mwandishi wetu
Baada ya kufungwa mabao 4-1 na Azam kwenye mechi ya Kombe la FA, Dodoma Jiji imedai inajipanga upya kuhakikisha inafanya vizuri watakapokutana na wapinzani wao hao tena kwenye mechi yao ya ligi inayofuata.
Dodoma ilikubali kipigo hicho juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kung’oka kwenye michuano hiyo, na sasa ikijiandaa na mechi ya ligi dhidi ya Azam Februari 4, mwaka huu.
Kocha msaidizi wa Dodoma, Kassim Liogope amesema walipambana kutafuta matokeo katika mechi hiyo lakini mabao mawili ya haraka haraka ya Azam ya kipindi cha pili yaliwamaliza kabisa licha ya juhudi zao za kutaka kuchomoa mabao hayo.
“Tulicheza vizuri lakini ni kama imetokea tu tumeshindwa, mabao mawili ya haraka haraka yalituchanganya, ukiangalia mchezo ulivyokuwa tulicheza vizuri na tuliwabana Azam ambao waliiona presha yetu kwao lakini yale mabao mawili yaliumaliza mchezo kabisa.
“Mechi hii imeisha lakini kwa sababu tuna mechi nao tena baada ya siku chache naamini mazuri ya hapa tumeyachukua na tutarekebisha tulipoteleza, tutaongeza umakini na kutakuwa na mechi nzuri sana tutakapocheza nao tena,” alisema Liogope.
Upande wa Kocha msaidizi wa Azam, Aggrey Morris alisema: “Mechi ilikuwa ngumu kweli kwa pande zote mbili, kipindi cha kwanza umakini ni kama ulipungua lakini nawapongeza vijana wamefanya kazi nzuri kama ilivyokuwa kipindi cha pili na mwisho tumeimaliza mechi.”
Dodoma ambayo pia ilipoteza mechi yao ya kwanza ya ligi dhidi ya Azam kwa mabao 2-1, katika mechi ijayo wao watakuwa wenyeji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Soka Dom Jiji yaisubiri Azam kwenye ligi
Dom Jiji yaisubiri Azam kwenye ligi
Related posts
Read also