Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji mpya wa Singida Big Stars, Ibrahim Ajibu ameahidi kupambana ili kutimiza ndoto za timu hiyo za kupambania ubingwa au kumaliza nafasi za juu huku akisisitiza kwamba haumizwi na maneno ya mitandaoni.
Ajibu ameeleza hayo akiwa miongoni mwa nyota wapya waliotua katika timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo akitokea Azam FC.
“Nafikiri mashabiki watarajie kuona mengi wanayoyahitaji kutoka kwangu ndivyo wavitarajie, kwa sababu nimekuja kupambana ili timu yetu igombanie ubingwa, kama itakosa basi tupate hata nafasi tatu za juu maana hakuna kinachoshindikana,” alisema Ajibu.
Pamoja na hayo, mchezaji huyo aliyewahi kukipiga Simba na Yanga pia alieleza kutoumizwa na maneno yanayoendelea mitandaoni na kwenye vijiwe mbalimbali kuhusu kutofanikiwa kucheza nje ya nchi licha ya kiwango kikubwa anachokionesha.
“Yaani mimi kwa kuniumiza sidhani kama yananiumiza kwa sababu siwasikiii wala siwafuatilii mambo yao ya Instagram sio mambo yangu hayo na hata hizo jumbe kama zinatumwa kwangu mimi sizioni kwa sababu sisomi hayo mambo.
“Na sijavunjika moyo kwa kuondoka Simba, Yanga wala Azam sababu sijazaliwa na hizo timu, nimezaliwa mtaani kwetu kwa hiyo kwingine napita tu, mpaka safari yangu ya mpira itakapoisha maana hata kwenda Ulaya hata shabiki anaweza kwenda kupitia biashara zake anazofanya kama anaona kwenda huko ni rahisi,” alisema.
Soka Ajibu: Ya mitandaoni hayaniumizi
Ajibu: Ya mitandaoni hayaniumizi
Related posts
Read also