Doha, Qatar
Baada ya kukumbana na maswali mengi kumhusu Cristiano Ronaldo, Kocha wa Ureno, Fernando Santos amesema umefika wakati kwa waandishi kuachana na maswali yanayomhusu mchezaji huyo.
Akizungumza jana Ijumaa, Santos alitoa ufafanuzi kwa mapana kuhusu mazungumzo yake na mchezaji huyo ambapo alifafanua namna alivyomwambia kwamba angeanzia benchi katika mechi ya hatua ya mtoano dhidi ya Switzerland.
Santos pia alilazimika kutoa ufafanuzu kuhusu kuwapo madai kwamba Ronaldo alitaka kuondoka kwenye kambi ya timu ya Ureno inayoshiriki fainali za Kombe la Dunia lakini baadaye alilazimika kusitisha maswali kuhusu mchezaji huyo wa zamani wa Man United.
“Nilizungumza naye baada ya chakula cha mchana siku ya mechi na kumualika ofisini kwangu, kwa sababu zilizo wazi kabisa Cristiano hakuwa na furaha kuhusu hilo, wakati wote amekuwa mchezaji wa kuanza kikosi cha kwanza,” alisema Santos.
“Baada ya kumwambia akaniambia, ‘unadhani hilo ni wazo zuri? Lakini tukawa na mazungumzo ya kawaida ambapo nilimuelezea kuhusu msimamo wangu na kimsingi alikubali, tukawa na mazungumzo mazuri na ya kawaida,” alisema.
“Hakuwahi kuniambia kwamba alitaka kuondoka kwenye timu ya taifa, na nadhani imetosha sasa tuache mazungumzo haya, aliamua kufanya mazoezi na wenzake na akafurahia mabao yote tuliyofunga, na mwishowe yeye ndiye aliyewaita wachezaji wenzake kujumuika pamoja na mashabiki na kuwashukuru,” alisema Santos.
“Tumuache Cristiano Ronaldo, katika kila mkutano na waandishi wa habari asilimia 90 ya maswali ni kuhusu Ronaldo, imetosha sasa tumuache. Kila mchezaji huchukia anapowekwa benchi, hilo ni jambo la kawaida, na makocha ni lazima wakabiliane na hali hiyo,” alisema
Santos katika hatua nyingine alisema kwamba milango ipo wazi kwa Ronaldo kurudi kwenye timu kwa ajili ya mechi ya robo fainali Jumamosi dhidi ya Morocco akisema kwamba itakuwa mechi nyingine tofauti.
Katika mkutano huo, Santos pia aliandamana na Joao Felix ambaye alisema kwamba wachezaji katika timu yao hawafurahii namna vyombo vya habari vinavyoripoti habari kumhusu Ronaldo huku akiwataka mashabiki wa Ureno kuwa na mashikamano.
Mechi za robo fainali Kombe la Dunia, leo Jumamosi
Morocco v Ureno
England v Ufaransa
Kimataifa ‘Maswali kumhusu Ronaldo yaachwe’
‘Maswali kumhusu Ronaldo yaachwe’
Related posts
Read also