Na mwandishi wetu
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amekimwagia sifa kikosi cha Mbeya City kwa soka safi walilolionesha kwenye mchezo wao wa jana ulioisha kwa sare ya mabao 2-2.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kocha huyo alisema hakutegemea kukutana na upinzani mkubwa kiasi hicho na hiyo ilitokana na utulivu iliyokuwa nao Mbeya City.
“Kikubwa niisifie Mbeya City kwa kweli wametusumbua, sikutegemea. Tumekutana na timu inacheza halafu inacheza kuanzia nyuma, ni timu ambayo lazima isumbue kwa kweli lakini nawapongeza pia vijana wangu wameonesha soka safi, wamepambana ingawa ilibidi tushinde lakini tumepata matokeo haya,” alisema.
Upande wa kocha msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima alisema wamepata matokeo hayo nyumbani kutokana na ugumu wa ligi ulivyo msimu huu kwa kila timu kujipanga vilivyo ingawa pia wanashukuru kwa kupata matokeo hayo.
“Kama nilivyosema ligi ni ngumu kila timu inajiandaa ndiyo maana wengine wanapata matokeo ugenini, nafikiri tuliiandaa timu kwa ajili ya kupata matokeo lakini mwisho wa dakika 90 imekuwa sare ya 2-2, tunashukuru Mungu kuliko kupoteza kabisa.
“Mpira ni mchezo wa makosa, lakini tunajitahidi kufanya marekebisho, siyo mwendelezo mzuri sana tulionao kwenye kutafuta matokeo katika mechi za hivi karibuni lakini tutaendelea kuongea na kuwarekebisha wachezaji ili tuimarike zaidi mechi zijazo,” alisema Mwamlima.
Soka Maxime aimwagia sifa Mbeya City
Maxime aimwagia sifa Mbeya City
Related posts
Read also