Na mwandishi wetu
Yanga SC imeshindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Kama ilivyo kawaida kwa Yanga msimu huu, iliwachukua mpaka kipindi cha pili kuandika bao la kuongoza kupitia mshambuliaji wao, Fiston Mayele aliyeandika bao hilo dakika ya 51 kupitia kwa mpira alioupiga nje ya 18 na kujaa wavuni.
Hata hivyo, iliwachukua dakika 16 kabla ya Hilal kuchomoa bao hilo kupitia kwa Mohamed Yousef baada ya Yanick Bangala kuokoa fyongo mpira wa krosi uliopigwa ndani ya 18 kabla ya mpira kumkuta mfungaji aliyepiga shuti lililomshinda kipa wa Yanga, Djigui Diarra.
Yanga iliyopania kutinga hatua ya makundi msimu huu kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, ilitawala kipindi cha kwanza kwa kupiga jumla ya kona saba kwa mbili dhidi ya wapinzani wao lakini pia walipiga mashuti mengi kwa wapinzani ikiwa ni mashuti mawili yaliyolenga lango wakati Hilal hawakupiga shuti lolote lililolenga lango.
Kipindi cha pili kilikuwa wazi kwa timu zote mbili kushambuliana kama vile Mayele ilivyobaki kidogo kuongeza bao la pili lakini mpira alioupiga uligonga mwamba na kurudi uwanjani, kama vile Abdulrahman alivyopiga mpira golini kwa Yanga wakati Diarra akiwa ametoka lakini mpira huo uliishia kuokolewa na Dickson Job.
Dakika ya 78, Mayele aliujaza wavuni mpira kwa kichwa akiunganisha krosi ya Djuma Shabani lakini mwamuzi alikataa bao kwa tafsiri kuwa alikuwa ameotea mpira huo na mpaka dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilimaliza kwa kutoshana nguvu.
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema bado wana nafasi ya kupindua matokeo na kufanya vizuri kwani wanakwenda kujipanga na kufanyia kazi makosa waliyoyaona wakihitaji kufanya vizuri zaidi kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa Oktoba 16, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan.
Timu nyingine ya Kipanga inayoiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika imetoka suluhu dhidi ya Club Africain ya Tunisia kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar wakati katika mechi nyingine ya michuano hiyo, Azam nao wamejikuta katika wakati mgumu ugenini baada ya kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Al Akhdar ya Libya.
Kimataifa Yanga, Al Hilal zatoka sare Kwa Mkapa
Yanga, Al Hilal zatoka sare Kwa Mkapa
Related posts
Read also