London, England
Mshambuliaji na nahodha wa zamani wa England, Alan Shearer ameisifu timu ya Arsenal akisema kwamba ni timu tofauti na ya siku za nyuma ingawa ameiweka kando katika mbio za kuliwania taji la Ligi Kuu England.
Shearer ambaye pia amewahi kutamba na klabu ya Newcastle, ameyasema hayo katika makala yake ya BBC akifafanua kwamba timu hiyo ni tofauti na timu ambayo mashabiki waliiona miezi takriban 13 iliyopita.
Ushindi wa mabao 3-0 ambao Arsenal iliupata Jumapili dhidi ya Brentford ni mwendelezo wa matokeo mazuri ya msimu huu kwa timu hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta.
Akifafanua Shearer alisema kwamba alitarajia Brentford kuwa kama ilivyokuwa katika mechi ya msimu uliopita walipoishinda Arsenal kwa mabao 2-0 lakini safari hii walikutana na Arsenal iliyokuwa tofauti japo walijaribu lakini haikuwa rahisi kwao.
“Kila kitu ni tofauti kwa Arsenal hii ya sasa kuanzia ushambuliaji, ulinzi, namna wanavyotawala mchezo pamoja na mwenendo mzima wa timu, wako makini katika kupata ushindi,” alisema Shearer.
Alisema kwamba Arsenal si tu ni timu kubwa na imara bali pia kuna hali ya uwajibikaji mzuri uwanjani na katika mechi na Brentford walikuwa vizuri kila eneo na walitawala mchezo kuanzia mwanzo.
Akiizungumzia kazi ya Arteta, Shearer alisema kwamba kocha huyo si tu kwamba ametengeneza timu tofauti lakini kwa ujumla amebadili hadi ari ya klabu na anahitaji kupongezwa kwa kazi hiyo kwa sababu alishutumiwa sana kwa namna alivyoanza vibaya msimu uliopita kwa vipigo vitatu mfululizo na kumaliza ligi wakiwa nafasi ya tisa.
Hadi sasa Arsenal imeshinda mechi sita kati ya saba za mwanzo na ndiyo inayoshika usukani wa ligi ingawa kwa maoni ya Shearer bado ni mapema kujiaminisha kwamba ina kasi ya kulipigania taji la Ligi Kuu England.
Kimataifa Shearer aisifu Arsenal, aitoa kwenye ubingwa
Shearer aisifu Arsenal, aitoa kwenye ubingwa
Related posts
Read also