Na Jonathan Haule
Simba imetangaza kuachana na beki wake wa kati, Paschal Wawa, mwamba huyu kutoka Ivory Coast si haba amefanya kazi kubwa tangu atue Simba msimu wa 2018/19 akitokea El Mereikh ya Sudan.
Wawa ambaye kabla ya kwenda El Mereikh alipita Azam, amekuwa mchezaji muhimu kwenye Ligi Kuu Bara na hata kwenye uwakilishi wa Simba katika michuano ya klabu Afrika.
Baada ya Wawa, mjadala ambao nimeuona umeanza kwenye mitandao ya kijamii kuanzia Facebook, Instagram na mengineyo, ni kuhusu mchezaji mwingine wa kuachwa Simba, na tayari baadhi ya watoa maoni wameanza kutaja majina.
Kwa haraka haraka tayari nimeona majina mawili, moja ni la John Bocco na lingine ni la Chris Mugalu, hawa tayari wameanza kutajwa na kuonekana kama muda walioitumikia Simba unatosha hivyo ni sahihi kwao kuondoka.
Hivi karibuni niliandika makala iliyochapishwa kwenye mitandao ya Green Sports kuhusu kilichoisibu Simba msimu wa 2021/22, nikabainisha vitu viwili kuwa ni kubweteka na mafanikio ya miaka minne mfululizo pamoja na mchoko unaowakabili baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.
Nikashauri umuhimu wa kuwaacha baadhi ya wachezaji na kuingiza wengine wenye ari mpya kuipigania Simba kazi ambayo kimsingi imeshaanza kufanywa katika siku za hivi karibuni kwani tayari usajili wa mastaa wapya Simba umeanza kufanywa.
Ukiniuliza mchezaji gani wa kuondoka Simba nami naweza kuwa na orodha yangu ndefu tu lakini kwa sasa hiyo ni kazi ya benchi la ufundi, tuendelee kushauriana, kuelekezana, kukosoana, kubishana mitandaoni huku tukishauri wa kuachwa na kubaki lakini uamuzi wa mwisho ubaki kwa Suleiman Matola na jopo lake.
Kumuacha au kutomuacha mchezaji kunahitaji kufanywa kwa kuzingatia sababu zinazojitosheleza, lazima benchi la ufundi ambalo watu wake wanaujua ukweli kuhusu mchezaji anayeachwa kwa kuwa wamekaa naye muda mrefu, wafanye uamuzi kwa kujiridhisha kwa nini wanaufanya.
Huu si mjadala wa kwanza kwenye mitandao kuhusu wachezaji wa Simba, hata Wawa alipojiunga na timu hiyo wapo ambao waliona klabu hiyo ilifanya kosa kubwa kwa kumsajili mchezaji huyo akionekana kuwa ni mzee na muda wake ulishapita, Wawa aliweza kuwathibitishia tofauti mashabiki hao.
Ni hivyo hivyo kwa Joash Onyango, Mkenya huyu licha ya kuja Simba akiwa ametoka kutwaa tuzo katika ligi ya Kenya, bado kwa baadhi ya mashabiki ilionekana kama Simba ilibugi kumsajili lakini kwa kipindi chote tangu ajiunge na Simba Onyango ameonyesha uwezo, si kwenye Ligi Kuu tu bali hata michuano ya klabu Afrika.
Kwa hali hiyo hata hii habari ya Mugalu na Bocco sisemi waachwe au wasiachwe bali nasisitiza, uamuzi wowote utakaofanywa usiwe wa kwenye mitandao bali kuwapo sababu za kiufundi za kuwaacha wachezaji hao, iwe ni kuchoka, uwezo kuwa chini, umri umewatupa mkono, hawana mchango unaoeleweka kwenye timu, isiwe anaachwa kwa sababu kumekuwa na kelele mitandaoni.
Nitatoa mfano mmoja kuhusu Bocco, amekuwa ni mchezaji wa kupanda na kushuka, anaposhuka kelele zinakuwa nyingi lakini akiibuka kidogo tu, yote yanasahaulika na kuonekana umuhimu wake, hakuna upembuzi wa kiufundi unaotolewa kuhusu mchezaji huyo badala yake anaposhuka kiwango tu habari ya kuachwa kwake inaanza.
Mfano ni hivi karibuni tu alipofunga bao kwenye mechi na Azam na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, mitandaoni hadithi ilibadilika, ikawa Bocco karudisha makali yake, nina hakika kwa mechi tatu zilizobaki za ligi ikitokea akafunga hata goli moja, tusishangae hadithi pia ikibadilika.
Msimu huu haukuwa mzuri kwa Bocco, kila mtu ni shuhuda katika hilo zikiwamo namba za mabao yake, mshambuliaji aliyekuwa na mabao 16 msimu uliopita sasa ligi ikielekea ukingoni ana mabao manne ni jambo lisilopendeza lakini tumejiuliza nini hasa tatizo? Ni mfumo wa timu haukumkubali kwa maana ya kwamba mfumo ukibadilishwa atakuwa vizuri au amefika mwisho kwa maana ya umri umeenda, vipi kuhusu makocha kubadilika.
Na vipi kuhusu mambo ya mchoko unaotokana na umri au kuwa timu moja muda mrefu na kulewa mafanikio, kwamba kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi amekuwa si Bocco yule mwenye kujituma kuwania tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.
Yote hayo yakijibiwa vyema na benchi la ufundi la Simba, usajili ujao unaweza kuwa mzuri si kwa Bocco na Mugalu tu bali kwa wote wanaotakiwa kuachwa, kabla ya kuamua sababu za kiufundi zipewe nafasi na si hamasa za mitandaoni.
Soka Baada ya Wawa nani mwingine?
Baada ya Wawa nani mwingine?
Related posts
Read also