Na mwandishi wetu
Youcef Belaili, nyota wa Algeria aliyeisumbua Uganda Cranes, Jumatano hii anatarajia kuiwakilisha Algeria kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi dhidi ya Taifa Stars.
Mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) ni ya pili kwa timu hizo za Kundi F baada ya ile ya kwanza ambayo Stars ilitoka sare ya ugenini dhidi ya Niger huku Algeria ikiwa nyumbani iliibugiza Uganda mabao 2-0.
Hapo kabla gumzo kwa timu ya Algeria alikuwa ni Ziyad Mahrez, winga huyu wa Man City alikuwa akitajwa kuwa angekuwa msumbufu katika mechi na Stars lakini baadaye ilibainika kwamba uwezekano wa mchezaji huyo kuichezea Algeria katika mechi hiyo haupo au mdogo.
Mechi ya Algeria na Uganda hata hivyo imethibitisha kwamba timu hiyo bado ina wachezaji wengi wakali na wanaoweza kuipa timu hiyo matokeo, mmoja wao ni Belaili, winga anayekipiga katika klabu ya Brest inayoshiriki Ligi 1 ya Ufaransa.
Katika ushindi wa Algeria dhidi ya Uganda, Belail alipika bao moja na kisha akafunga la pili kwa juhudi binafsi baada ya kuivuruga kwa chenga safu ya ulinzi ya Uganda kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Belail ambaye pia ni mshambuliaji, ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha Algeria kutwaa taji la Afcon mwaka 2019 na mwaka jana alikuwamo katika kikosi cha Algeria kwenye michuano ya Fifa Arab Cup iliyofanyika Qatar na kuifungia bao lililoipeleka timu hiyo fainali katika mechi dhidi ya Qatar.
Historia ya Belail ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 30, hata hivyo iliingia doa mwaka 2015 alipofungiwa na CAF kwa miaka miwili baada ya kufanyiwa vipimo katika moja ya mechi na majibu kuonyesha kwamba alitumia cocaine.
Inadaiwa alikutwa na kosa hilo mara ya pili miezi kadhaa baadaye na hivyo kufungiwa huku klabu ya USM Alger aliyokuwa akiichezea kusitisha mkataba naye kutokana na kosa hilo ingawa kwa sasa yote hayo ameyaweka kando na amebaki kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Algeria.
Akiizungumzia mechi na Algeria, kocha wa Stars Kim Poulsen ameshasema kwamba wanajua kwamba wanaingia uwanjani kushindana na timu bora na hivyo wataingia uwanjani na mkakati wa kudhibiti ubora wa Algeria.
Kauli ya Poulsen inatoa ishara ya mchezo kutawaliwa na mbinu zaidi na hapana shaka mbinu hizo ndizo zinazoweza kuisaidia Stars ambayo inacheza na timu bora na ambayo tayari imedhihirisha ubora wake katika mechi yao na Uganda.
Kimataifa Si Mahrez tu, Algeria wana Belail
Si Mahrez tu, Algeria wana Belail
Related posts
Read also