Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga umewataka mashabiki na wadau wake kuunganisha nguvu na kusahau matokeo ya sare za mechi zao tatu mfululizo zilizopita ili kuhakikisha wanarejea kwenye njia yao ya kuutwaa taji la Ligi Kuu ya NBC Bara mapema.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ameyasema hayo leo huku akiongeza kuwa kuwa timu hiyo imeingia kambini jana tayari kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na hiyo itakuwa fursa kwao kupata ushindi na kuendeleza wimbi la kutwaa ubingwa msimu huu.
Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 57 dhidi ya Simba inayofuatia ikiwa na pointi 49, imetoka suluhu mechi zake tatu zilizopita dhidi ya Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons na kuanza kuibua hofu kwa baadhi ya mashabiki kwamba matokeo hayo yanauweka rehani ubingwa huo walioukosa kwa misimu minne mfululizo sasa.
“Hayakuwa malengo ya kupata pointi moja lakini ndiyo imetokea na ndipo ugumu wa ligi unapoonekana ndiyo maana tunaambiwa Wanayanga kwamba tuendelee kushikamana, tusonge mbele.
“Kauli yetu Yanga ni daima mbele nyuma mwiko, najua matokeo haya yametuathiri lakini yamaeshapita na ili tusiathirike zaidi inapaswa kuungana kuona tunafanyeje ili tupate matokeo mazuri zaidi siku zinazokuja.
“Matokeo haya yametupa changamoto na changamoto ni kipimo cha maarifa kwa binadamu kwa hiyo hatupaswi kuanza kulumbana, tukianza hivyo maana yake tutakuwa tumepungukiwa maarifa, kwa hiyo Wanayanga tusitoke kwenye ligi bado tunautazamia ubingwa na tunaongoza, tuendelee kushikamana,” alisema Bumbuli.
Bumbuli aliongeza kuwa nguvu hiyo inapaswa kuunganishwa zaidi kuelekea mchezo wao na Dodoma, akiwasihi Wanayanga kuhamasika na mchezo huo lengo likiwa ni kupata matokeo kwenye mechi saba zilizobaki ili watangaze ubingwa mapema ikiwa tayari benchi la ufundi la timu hiyo limeshajua wapi pa kurekebisha ili waendelee na wimbi la ushindi.
“Benchi la ufundi limeona changamoto zilizojitokeza kwenye mechi tatu zilizopita na watayafanyia kazi kuona yale yaliyojitokeza huko nyuma hayajirudii kwenye mechi yetu inayofuata na nyingine zilizosalia, wadau na mashabiki pia wanajua wapi tumekwama kwa hiyo tupo kwenye kurekebisha hayo yote ili tuwe vizuri kwenye mechi ya Dodoma na zinazofuata,” alisema Bumbuli.
Soka Bumbuli awatuliza mashabiki Yanga
Bumbuli awatuliza mashabiki Yanga
Related posts
Read also