Roma, Italia
Mshambuliaji wa Ubelgiji, Romelu Lukaku amejiunga na klabu ya Roma ya Italia kwa mkopo akitokea Chelsea huku kukiwa na habari kwamba alikataa ofa ya kwenda kucheza soka Saudi Arabia.
Lukaku anarudi kwa mara nyingine katika Ligi ya Serie A nchini Italia baada ya kuwa na Inter Milan ambayo aliiwezesha kufikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Mapokezi ambayo klabu hii na mashabiki wamenipa ni mambo yaliyonivutia na inakuwa kama hamasa ya kuendelea zaidi kujitoa kwa kila hali na timu yangu mpya,” alisema Lukaku.
Habari za ndani zinadai kwamba Lukaku mwenye umri wa miaka 30 amekubali kupunguziwa mshahara ili tu apate nafasi ya kuungana na kocha Jose Mourinho ambaye ndiye anayeinoa timu hiyo kwa sasa.
Mourinho aliwahi kuwa na Lukaku katika klabu ya Chelsea msimu wa 2013-14 na mwaka 2017 kwa mara nyingine, Mourinho akiwa Man United alimsajili mchezaji huyo kwa ada ya Pauni 75 milioni kutoka klabu ya Everton.
“Nilipata fursa ya kuzungumza na mmiliki na niliguswa na shauku yao, sasa tunatakiwa kufanya kazi, tutulie na kuwa bora mechi baada ya mechi, kwa upande wangu sina cha kusubiri kabla ya kujitoa kwa ajili ya wachezaji wenzangu ndani na nje ya uwanja,” alisema Lukaku..
Mwaka 2019, Lukaku alisaini mkataba wa kudumu Inter Milan kwa ada ya Pauni 74 milioni akitokea Man United lakini mwaka 2021 alirudi Chelsea waliomsajili kwa ada ya Pauni 97.5 milioni lakini hakuwa na mafanikio na mara ya mwisho kuonekana akiiwakilisha timu hiyo ilikuwa ni Mei 2022.
Lukaku hakuwa katika mpango wa kocha mpya wa Chelsea, Mauricio Pochettino na hakusafiri na timu hiyo katika ziara za maandalizi ya msimu wa 2023-24 nchini Marekani na hilo linadaiwa kuchangia kumfanya aihame timu hiyo.