Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa KMC, Thierry Hitimana ameeleza wazi hofu yake wakati wakijipanga kuivaa Mbeya City katika mchezo unaotarajia kupigwa kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Hitimana ambaye aliwahi kuwa kocha Simba, amefafanua kuwa wanapaswa kuwa makini katika mchezo huo kutokana na ubora wa timu wanayokutana nayo, upinzani wa timu za kushuka daraja unavyoshindwa kutabirika lakini pia ubora hafifu wa ulinzi wa timu yake.
Kocha huyo ameongeza kwamba wapinzani wao hao wamekuwa kwenye kiwango kizuri na matokeo ya ushindi hivi karibuni, hali ambayo imewafanya wawe wenye kujiamini kabla ya kucheza nao bila ya kujali kigezo cha kwamba wao ndiyo wenyeji kwenye mechi hiyo.
“Haijalishi sana kama sisi ndiyo wenyeji lakini wapinzani wetu wameonesha kiwango hivi karibuni na matokeo waliyoyapata yamewapa nguvu mno, kabla ya kudroo na Polisi Tanzania walipata ushindi dhidi ya Azam kwa hiyo unaona namna gani hiyo inawapa morali dhidi yetu.
“Kingine sisi tuna pointi 28 kwenye nafasi ya nane, pointi mbili tofauti na waliopo nafasi za chini za kushuka daraja kwa hiyo tunahitaji ushindi kwenye mazingira magumu dhidi ya timu ngumu na ndipo unapoona ugumu wa mechi yetu halafu pia tuna tatizo la kuruhusu bao kwenye mechi mfululizo zilizopita, hilo nalo linaweza kuwa tatizo kwetu.
“Lakini tunaendelea kujipanga vilivyo kuona tunatokaje hapa na tunakaaje vizuri kwa kuhakikisha tunatoka kwenye kuvutwa nafasi za chini kabla ya kuwaza namna gani tunamaliza katika nafasi za juu,” alisema Hitimana.
Hata hivyo, Mbeya City inayoshikilia nafasi ya nne kwa pointi zake 32 ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza msimu huu iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Soka Hitimana aihofia Mbeya City
Hitimana aihofia Mbeya City
Related posts
Read also