Na mwandishi wetu
Azam FC inatarajia kujipima na Al Hilal ya Sudan ikiwa ni mchezo wao wa kwanza wa kirafiki wa kimataifa katika kambi waliyoko nchini Tunisia.
Ofisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe (pichani) alisema wanatarajia kuumana na timu hiyo keshokutwa Ijumaa kabla ya kucheza mechi nyingine tatu kati ya Esperance, US Monastir na CS Sfaxien.
Ibwe alisema katika siku mbili walizokuwa nchini humo kocha wao Mkuu, Yousouph Dabo amekuwa akikazia mazoezi ya pumzi na utimamu wa mwili na mazoezi yao wamekuwa wakifanya kwa nyakati mbili kwa siku.
“Unajua wachezaji wametoka kwenye mapumziko sasa ingawa tulianza kidogo mazoezi huko nyumbani lakini tulivyofika huko kocha ameendelea nayo mazoezi ya pumzi na utimamu wa mwili uzuri kwamba hoteli tuliyofikia kuna gym na uwanja hapahapa,” alisema Ibwe.
“Pamoja na ugumu wa mazoezi hayo lakini Ijumaa tutacheza mechi moja dhidi ya mabingwa wa Sudan, Al Hilal na baada ya siku mbili tutacheza mechi nyingine mbili hadi tatu na timu kubwa za huku kama Esperance, US Monastir na CS Sfaxien,” alisema Ibwe.
Alisema lengo la kutaka kucheza na timu kubwa ni kutokana na aina ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika wanayotarajia kushiriki kuanzia Agosti, mwaka huu huku mikakati yao ikiwa ni angalau kufika hatua ya makundi.
Pia alifafanua kwamba tangu wafike Tunisia, Dabo amevutiwa na uwajibikaji na juhudi zinazooneshwa na wachezaji, akiamini baada ya kukamilika kwa kambi hiyo ya siku 21, Azam itakuwa tayari kwa kuwania mataji msimu ujao.
Azam FC ni miongoni mwa timu mbili kubwa nchini ambazo zimefanya usajili mkubwa baada ya kumaliza bila taji lolote katika misimu miwili iliyopita.