Na mwandishi wetu
Nahodha wa Simba, John Bocco amesema ana imani kubwa na wachezaji wapya waliosajiliwa hivi karibuni na timu hiyo kwamba watawasaidia kufikia malengo yao msimu huu.
Kauli ya nahodha huyo inakuja kutokana na viwango vinavyooneshwa na wachezaji hao katika mechi za ligi ambazo wameshacheza hadi sasa.
Katika dirisha la usajili la Januari lililofungwa hivi karibuni, Wekundu hao waliwasajili wachezaji wanne ambao ni Saido Ntibazonkiza, Ismail Sawadogo, Jean Baleke na Mohammed Mussa.
Bocco ameeleza kuwa kwa muda mfupi tangu wachezaji hao wajiunge na timu hiyo wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chao ikiwemo kuwasaidia kuwapa ushindi katika baadhi ya mechi za ligi.
“Angalia Ntibazonkiza na Baleke wote wameshafunga mabao ambayo yameipa timu pointi tatu lakini Sawadogo alicheza vizuri kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji, naamini uwepo wao utatusaidia kufikia malengo ambayo tumekusudia kuyafikia msimu huu,” alisema Bocco.
Mshambuliaji huyo anayeshika nafasi ya pili kwa ufungaji kwenye kikosi cha timu hiyo msimu huu ameeleza kuwa kasi waliyoanza nayo wachezaji hao inaendana na matarajio yao hasa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo lengo lao ni kufika nusu fainali.
Bocco alisema kitu cha msingi ni kuendelea kuwapa ushirikiano wachezaji hao ili waweze kuzowea mapema mazingira ya timu ikiwemo mifumo na hatimaye kutoa mchango mkubwa zaidi ya ule wanaoutoa hivi sasa.