London, England
Kocha wa Chelsea, Graham Potter amefarijika baada ya timu yake kuifunga Craystal Palace bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) huku akifurahia usajili wa mshambuliaji wake mpya, Mykhailo Mudryk.
Potter amekuwa katika kipindi kigumu akiwa na rekodi ya ushindi wa mechi mbili tu kati ya 10 zilizopita za EPL lakini Jumapili hii walau amepata cha kujifariji kwa ushindi huo uliotokana na bao la kichwa la Kai Havertz katika dakika ya 65 na kuwa ushindi wa kwanza wa timu hiyo kwa mwaka 2023.
Chelsea iliingia uwanjani kuikabili Palace ikiwa inaandamwa na janga la wachezaji majeruhi ambapo pia Potter amethibitisha kwamba mchezaji wake, Denis Zakaria atakosekana uwanjani kwa wiki nne.
“NItakuwa naongopa kama sitasema kwamba nimefarijika lakini ni jambo zuri kupata ushindi nafikiri tulicheza vizuri kuliko ilivyokuwa kwa Fulham tulipotoka bila point na hapo hapo Joao Felix anapewa kadi nyekundu lakini kuna kitu tumefanya hapa,” alisema Potter.
Mechi ijayo ya Chelsea itakuwa Jumamosi dhidi ya Liverpool, mechi ambayo Potter huenda akamtumia Mudryk, nyota mpya kutoka Ukraine aliyesajiliwa kwa Euro 70 milioni ambaye katika mechi na Palace alikuwa jukwaani usajili wake ukiwa umekamilika mapema siku hiyo hiyo.
Arsenal pia ilikuwa na nia ya kumsajili Mudryk aliyekuwa akikipiga Shakhtar Donetsk kabla ya kupigwa bao na Chelsea iliyokamilisha dili hilo haraka haraka.
Alipoulizwa kuhusu kuendelea kufanya usajili akiwa tayari amekamilisha usajili wa wachezaji wanne, Potter alisema kwamba hilo ndilo jambo analolifikiria wakati wowote hasa kwa kuwa soka ni mchezo ambao ukiufanyia tathmini utaona jinsi matokeo yanavyoamua kila kitu.