Na mwandishi wetu
Ikimtumia kwa mara ya kwanza nyota wake mpya Saido Ntibazonkiza, leo Ijumaa, Simba imeitembezea ubabe Prisons kwa kuinyuka mabao 7-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unakuwa umeiimarisha Simba katika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo ikiwa imefikisha pointi 44 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 47 lakini Simba ikiwa imecheza mechi 19 wakati Yanga imecheza mechi 18 na kesho itajitupa uwanjani kukabiliana na Mtibwa.
Jambo jingine zuri ni kwamba Simba sasa inakuwa imefikisha jumla ya mabao 47 ya kufunga na kuwa ndiyo timu yenye mabao mengi ya kufunga kwenye ligi hiyo ikifuatiwa na vinara Yanga ambao hadi sasa wana mabao 36 ya kufunga.
Nahodha wa Simba John Bocco naye ana kila sababu ya kujivunia matokeo hayo akiwa amefunga mabao matatu peke yake yaani hat trick na hivyo kufikisha mabao tisa ya ligi akiwa ametanguliwa na nyota mwenzake wa Simba, Moses Phiri mwenye mabao 10 ambaye kwa sasa ni mgonjwa na atakuwa nje kwa wiki kadhaa.
Mafanikio hayo ya Bocco ni kama vile kumkumbusha Fiston Mayele akaze buti kwani ndiye kinara wa mabao wa ligi hiyo akiwa ametupia kambani mara 14.
Sambamba na hilo, Ntibazonkiza aliyejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Geita Gold, ameanza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya Simba kwa mguu mzuri baada ya kufunga mabao matatu kama ilivyo Bocco na huo kuwa mwanzo mzuri kwake katika kikosi cha Simba.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga ni kama vile alianza kujitabiria mapema mafanikio katika kikosi cha Simba kwani baada ya usajili wake kukamilika aliwaahidi makubwa wana Simba lakini akasema hana sababu ya kusema mengi badala yake iachwe miguu izungumze na ndicho kilichotokea leo katika mechi na Prisons.
Bao la saba la Simba lilifungwa na Shomari Kapombe wakati bao pekee la Prisons lilifungwa na Jeremiah Juma.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, Singida Big iliichapa Geita Gold mabao 2-1 wakati Dodoma Jiji iliilaza Kagera Sugar mabao 2-0.
Soka Simba yainyuka Prisons 7-1
Simba yainyuka Prisons 7-1
Related posts
Read also