Na mwandishi wetu
Kamati ya Uchaguzi ya klabu ya Simba imetangaza uchaguzi mkuu wa viongozi wa klabu hiyo ambao utafanyika Januari 29 mwakani.
Taarifa kuhusu uchaguzi huo imewekwa wazi leo baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kutangaza majina ya wajumbe wa kamati hiyo ambayo iliteuliwa kwenye kikao cha bodi hiyo kilichoketi hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Kamati ni Boniface Lihamwike na makamu wake ni Mwajuma Choggy huku wajumbe wakiwa ni Richard Mwalibwa, Gerald Mongela na Juma Simba.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Lihamwike alitangaza tarehe hiyo na kuujulisha umma na mashabiki wa Simba kuwa safari hii uchaguzi utafanyika kupitia kanuni za uchaguzi za Simba na si za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama ilivyokuwa awali.
“Nichukue nafasi hii kuutangazia umma, wanachama na mashabiki wa Simba kuwa tarehe ya uchaguzi ni Januari 29, mwakani lakini pamoja na hilo pia niwaeleze kwamba safari hii kanuni za uchaguzi zitakazotumika ni za Simba SC.
“Awali kwenye chaguzi zilizopita Simba ilikuwa ikitumia kanuni za TFF kwa sababu ilikuwa haijapata kanuni zake, zilikuwa bado hazijatengenezwa na katiba ya Simba inaruhusu kutumia kanuni za TFF kabla ya bodi kuona zitengenezwe kanuni zetu zitakazotumika kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi,” alisema Lihamwike.
Mwenyekiti huyo pia alieleza kanuni muhimu ya sita ya uchaguzi huo yenye vigezo vya wagombea ambapo kwa upande wa mwenyekiti awe mwadilifu, kiwango cha juu cha uaminifu, haiba ya kuwakilisha klabu ndani na nje ya nchi angalau awe na shahada ya chuo kikuu na awe mwanachama hai wa Simba.
“Nafasi ya ujumbe wa bodi ya wakurugenzi, lazima awe amefika kidato cha nne, uzoefu uliothibitishwa wa angalau miaka mitatu ya uongozi wa soka. Asiwe amepatikana kamwe na hatia ya kosa la jinai au kifungo bila faini, awe na miaka 25 na asizidi miaka 65 na asiwe mmiliki au mwenye hisa za klabu nyingine ya soka au mwamuzi wa soka,” alifafanua.
Aidha, mjumbe Mongela alitaja zoezi la kuchukua fomu litafanyika katika ofizi za klabu, zikianza kutolewa Desemba 5 saa 3 asubuhi mpaka Desemba 19, mwaka huu saa 10 jioni.
“Desemba 20-21, 2022 itakuwa ukaguzi wa fomu zilizorudishwa ndani ya muda, Desemba 22-24, 2022 itakuwa ni usajili wa watia nia, Desemba 28, 2022 itakuwa kubandika majina ya wagombea waliopita kwenye usaili.
“Desemba 29-20, 2022 tutatoa muda wa kupokea mapingamizi dhidi ya wagombea. Januari Mosi mpaka Pili, 2023 itakuwa ni kupitia mapingamizi, kutoa wito kwa walioweka mapingamizi na wagombea waliowekewa mapingamizi.
“Na Januari 3 mpaka 4, 2023 tutakuwa na kipindi cha kusikiliza mapingamizi na kutoa uamuzi halafu Januari 5 tutatangaza majina ya wagombea, Januari 6 mpaka 26 itakuwa dirisha la kampeni kwa waliopita kugombea na Januari 29 itakuwa uchaguzi” alisema Mongela.
Simba ilifanya uchaguzi wake wa mwisho Novemba 5, 2018 na kumchagua Swed Nkwabi kuwa mwenyekiti ambaye alidumu mwaka mmoja kabla ya kung’atuka na kuchaguliwa Murtaza Mangungu aliyepo sasa.
Soka Uchaguzi Simba Januari mwakani
Uchaguzi Simba Januari mwakani
Related posts
Read also