Na mwandishi wetu
Ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars umemfurahisha kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi lakini amesisitiza kuwa bado hajawafikia kwenye kiwango na ubora wanaouhitaji ndani ya kikosi hicho.
Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi huo jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kurejea kileleni kwa pointi 26 sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili, lakini Yanga ikiwa juu kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Nabi alifafanua kuwa ingawa walipata muda mchache wa maandalizi lakini anafurahi kuona wachezaji wake walitambua umuhimu wa mchezo huo, wakafanya kile alichowaelekeza na kubaki kwenye njia salama ya kutetea ubingwa wao.
Alisema ingawa japokuwa wameibuka na ushindi lakini bado wana sehemu nyingi za kurekebisha makosa ili kufikia malengo ya ubora wanaoutaka ndani ya kikosi hicho kulingana na mechi ngumu na michuano mikubwa inayowakabili msimu huu.
“Japo tumepata ushindi huo haimaanishi kwamba muda wote tulicheza vizuri zaidi, vipo vingi vya kusahihisha, kwa kuwa tunacheza Kombe la Shirikisho Afrika mechi zinazidi kuwa ngumu, hivyo lazima kuna makosa turekebishe ili timu ifike tunapopataka.
“Bado hatujafika kwenye malengo tunayoyataka kwamba timu ni bora lakini bado tunaendelea kujitahidi kuhakikisha timu inakuwa bora zaidi ya hapa kwa ajili ya michuano na mechi ngumu zilizo mbele yetu,” alisema Nabi.
Kocha wa Singida, Hans Pluijm naye aliipongeza Yanga kwa uwezo mzuri waliounesha lakini pia alisema ulichangiwa na kikosi chake kutokuwa na mbinu bora, nidhamu na kuwapa nafasi wapinzani wao kuutawala mchezo.
“Nafikiri niipongeze Yanga kwa sababu walitumia nafasi ya kucheza na tukawa tofauti kimchezo kuanzia mbinu, nidhamu na tukapambana kusawazisha mambo uwanjani lakini haikusaidia kitu, nadhani ilikuwa siku mbaya sana kwetu.
“Simba na Yanga ndiyo timu kubwa, tunahitaji kupambana na kuwapa changamoto lakini kwenye mechi hii haikuwa vile tulivyopanga. Hakukuwa na ushirikiano kwa mabeki, viungo na washambuliaji, kulikuwa na nafasi kubwa kati yao, hicho ndicho kilichoipa nafasi na muda Yanga wa kuumiliki mchezo na hilo ndilo lilikuwa tatizo letu,” alisema Pluijm.
Soka Nabi hajaridhika na kiwango Yanga
Nabi hajaridhika na kiwango Yanga
Related posts
Read also