Na mwandishi wetu
Simba, ikiwa chini ya kocha Juma Mgunda imeendeleza ubabe kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Nyasa Big Bullets ya Malawi mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa leo kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba sasa inakuwa imewatoa mashindanoni Wamalawi hao na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kuanza na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya awali ambayo timu hiyo ilikuwa ugenini nchini Malawi.
Kwa ushindi huo, Simba sasa inasubiri kuumana na timu mojawapo kati ya Red Arrows ya Zambia au Fast De Agosto ya Angola katika hatua inayofuata.
Alikuwa ni kiungo mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri aliyeihakikishia timu hiyo ushindi kwa mabao aliyofunga katika dakika za 29 na 50.
Mafanikio hayo pamoja na mambo mengine pia yanazidi kuing’arisha nyota ya kocha Mgunda ambaye alichukuliwa kutoka Coastal Union baada ya kuondoka kwa Zoran Maki japo bado ni mapema mno kwani safari ya timu hiyo kwenye michuano hiyo yenye utajiri inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ndio kwanza inaanza.
Katika mechi ya leo, Mgunda alifanya mabadiliko kadhaa ikiwamo kumpa nafasi mshambuliaji Dejan Georgejivic au ‘Mzungu’, mabadiliko ambayo kiujumla yalionekana kama ni sehemu ya mbinu za kiufundi zaidi za kocha huyo ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Coastal.
Soka Simba yapiga hatua CAF
Simba yapiga hatua CAF
Related posts
Read also