Paris, Ufaransa
Mathias Pogba ambaye ni kaka wa kiungo wa Juventus, Paul Pogba inadaiwa amekamatwa na tayari ameanza kuhojiwa akihusishwa na tuhuma za mpango wa kujiingizia fedha kwa njia zisizo halali kutoka kwa ndugu yake.
Mbali na Mathias, watu wengine wanne pia wamekamatwa na kuanza kuhojiwa wakihusishwa na uhalifu huo na tuhuma nyingine za mtandao wa uhalifu huo wa kijinai ingawa wakili wa Mathias, Yassine Bouzroe amesema kwamba mteja wake hana kosa lolote.
Mathias hata hivyo aliwahi kukiri kuhusika katika video iliyokuwa kwenye mitandao ya kijamii mapema mwezi uliopita akiahidi kutoa ushuhuda kuhusu mambo mbalimbali ya ndugu yake ambaye pia amewahi kuichezea klabu ya Man United.
Waendesha mashitaka nchini Ufaransa walianza taratibu za uchunguzi mapema mwezi uliopita baada ya Paul kudai kwamba anawindwa na genge maalum lenye nia ya kumtisha na kumchafua. Paul awali aliwasilisha madai hayo katika mamlaka za mjini Turin akidai kwamba kuna genge ambalo linataka kujipatia Euro 13 milioni kutoka kwake kwa njia zisizo halali.
Paul ambaye alikuwa na timu ya Ufaransa iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 2018, alihamia Juventus akiwa mchezaji huru akitokea Man United ingawa kabla ya hapo aliwahi kuichezea timu hiyo wakati ndugu yake Mathias naye ni mwanasoka profesheno ambaye amewahi kuchezea klabu mbalimbali barani Ulaya pamoja na timu ya Taifa ya Guinea.
Kimataifa Ndugu wa Pogba akamatwa, ahojiwa
Ndugu wa Pogba akamatwa, ahojiwa
Related posts
Read also