Madrid, Hispania
Klabu ya Atletico Madrid ya Hispania inadaiwa kuanza kumpigia hesabu Cristiano Ronaldo ili imsajili kwa ajili ya msimu wa 2022/23 ambao unatarajia kuanza baadaye mwezi ujao.
Habari nchini Hispania zinadai kuwa vigogo wa klabu hiyo wameanza kuwasiliana na wawakilishi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 ili kuangalia wanachoweza kufanya ili ajiunge na timu hiyo mahasimu wa timu yake ya zamani ya Real Madrid.
Uamuzi wa Atletico kumtaka Ronaldo unamfanya mchezaji huyo ambaye tayari amekataa ofa inayodaiwa kuwa na maslahi makubwa ya kwenda kucheza soka Saudi Arabia, aamue ama kubaki Man United au kujiunga na timu hiyo.
Timu nyingine zilizodaiwa kumtaka za Spartak Moscow, Chelsea na Bayern Munich zimeamua kuachana naye, kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amesema hivi karibuni kwamba hawana tena mpango wa kumsajili Ronaldo kauli inayoonekana kufanana na ile ya mtendaji mkuu wa Bayern, Oliver Kahn wakati Spartak imemtoa kabisa mchezaji huyo katika hesabu zao.
Ronaldo ni wazi kwamba atafurahia kujiunga na Atletico, timu ambayo itampa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, nafasi ambayo anaikosa Man United huku ikidaiwa kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa inayomfanya atake kuondoka katika klabu hiyo ambayo imemaliza Ligi Kuu England ikiwa nafasi ya sita wakati Atletico imemaliza ikiwa nafasi ya tatu katika La Liga.
Atletico hata hivyo inaweza kukwama kumpata mchezaji huyo kutokana na uamuzi wa kocha mpya wa Man United, Erik ten Hag ambaye ameshasema kwamba Ronaldo ataendelea kuwa katika klabu hiyo ya Old Trafford hata baada ya mkataba wake wa sasa wa mwaka mmoja kumalizika.
Kikwazo kingine pia kinaweza kuwa masuala ya fedha kwani zipo habari kwamba baadhi ya vigogo wa Atletico usajili wa Ronaldo unawapa tabu wakihofia kuiweka klabu yao katika wakati mgumu hasa wanapoufikiria mshahara mkubwa wa mchezaji huyo hapo hapo wana hofu ya dau kubwa la uhamisho kutoka Man United na hivyo kujikuta wanavuruga bajeti yao kwa sababu ya mchezaji huyo mmoja.
Kimataifa Atletico Madrid yamtaka Ronaldo
Atletico Madrid yamtaka Ronaldo
Related posts
Read also