New York, Marekani
Mastaa wa filamu, Jennifer Lopez na Ben Affleck wamefunga ndoa Jumamosi hii mjini Las Vegas ikiwa ni miaka 17 imepita tangu wafute mpango huo wakati ambao mapenzi yao yalikuwa motomoto na kuwa gumzo duniani kote hadi kubatizwa jina la Super Couple.
“Tumefanya kweli, mapenzi ni matamu, mapenzi ni uungwana, na pia mapenzi yamekuwa ni uvumilivu, ni miaka 20 ya kuvumiliana, walikuwa sahihi waliosema kati ya vyote mtu anahitaji mapenzi,” aliandika Jennifer au J.Lo katika mtandao wa kijamii wa mashabiki wake wa OntheJLo akizungumzia kurudiana kwao baada ya kuachana mwaka 2004.
J.Lo pia aliandika kuwa yeye na Ben walisafiri kuelekea Las Vegas Jumamosi na kupanga foleni ya kupewa cheti cha ndoa pamoja na wapenzi wengine wanne waliokuwa wakisubiri zamu yao huku ikidaiwa kwamba J.Lo sasa anapanga kubadili jina ambapo ataitwa Jennifer Affleck.
Habari za J.Lo na Ben kurudiana zilipotoka mwaka jana zilikuwa kivutio kwa mashabiki wao ambao walianza kutuma salamu kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wao wakiwapongeza kwa uamuzi huo ingawa haikutarajiwa kama wangefikia hatua ya kufunga ndoa.
Asubuhi baada ya ndoa kufungwa, J.Lo alitupia picha yake mitandaoni akiwa kitandani na pete mpya ya ndoa huku akisema katika hali ya furaha, “Tuna furaha isiyo kifani, familia inayopendeza ya watoto watano wa kipekee na tuko katika maisha ambayo hatujawahi kuwa nayo, yanayotufanya tuwe na kila sababu ya kuyafurahia yajayo.”
Mbali ya kutajwa kuwa ni Super Couple, wawili hao pia wakati mapenzi yakiwa moto moto walibatizwa jina la Bennifer huku wakifuatiliwa kila hatua waliyopiga na vyombo vya habari jambo ambalo inadaiwa lilikuwa likimkera J.Lo na kutajwa kuwa sababu mojawapo ya kuachana kwao.
Hadithi ya J.Lo na Ben katika mapenzi ilianzia mwaka 2002 wakati wakiigiza filamu ya Gigli kabla ya kuchumbiana mwaka 2003 huku wakitarajiwa kufunga ndoa wakati wowote kuanzia hapo lakini mwaka uliofuata mpango huo ulivunjika katika namna ambayo haikutarajiwa.
Kwa J.Lo hii inakuwa ndoa yake ya nne, alifunga ndoa na mwanamuziki mwenzake Marc Anthony mwaka 2004 mara tu baada ya kuachana na Ben na kwa pamoja wana watoto wawili mapacha kabla ya kuachana mwaka 2014, Ben naye alifunga ndoa na mcheza filamu Jennifer Garner ndoa iliyofungwa mwaka 2005 na kuvunjika mwaka 2018, na kwa pamoja wana watoto watatu.
Burudani J.Lo Ben Affleck wafunga ndoa
J.Lo Ben Affleck wafunga ndoa
Related posts
Read also