Na mwandishi wetu
Kamati ya Maadili ya TFF imesogeza mbele kesi ya ukiukwaji maadili inayomkabili Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara na sasa itasikilizwa tena Julai 20, mwaka huu.
Uamuzi huo umefikiwa kutokana na pingamizi lililowekwa na mwanasheria wa Manara, Charles Tumaini ambapo katika pingamizi hilo wakili huyo amedai kuwa kanuni zilizotumika kufungua shauri hilo dhidi ya Manara pamoja na adhabu zake hazitumiki kwa kuwa bado hazijasaliwa na mamlaka husika.
Tumaini amefafanua kuwa katika kikao hicho kilichofanyika juzi waliwasilisha mapingamizi mawili, moja likiwa ni kuilalamikia mamlaka iliyomshtaki haina nguvu ya kufanya hivyo lakini hilo lilitupiliwa mbali.
“Kamati iliondoa pingamizi letu la kwanza na kusema halina mashiko lakini la pili ni kuhusu kanuni zilizotumika kumshitaki mteja wetu zilikuwa zina walakini kwa kuwa kanuni hizo zilipaswa kuwa zimesajiliwa na mamlaka husika kwenye Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na tuligundua hazikuwa zimesajiliwa, tuikaweka pingamizi kanuni hizo haziwezi kutumika mpaka zisajiliwe,” alieleza Tumaini.
“Pingamizi la pili, tulilisikiliza kwa maana ya upande wetu na upande wa pili. Kimsingi tulifikia mwisho kwamba tusubiri hadi Julai 20, mwaka huu, saa sita kwa ajili ya uamuzi mdogo kuhusu mapingamizi yetu hayo hasa hilo moja kama tutakuwa tumefanikiwa basi tutakwenda kwenye kusikilizwa kama ambavyo alisomewa,” alisema.
Manara ameingia kwenye shauri hilo baada ya kutokea sintofahamu Julai 2, mwaka huu wakati wa mechi ya fainali ya Kombe la FA iliyozikutanisha Yanga na Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha akionekana kwenye video akizozana na Rais wa TFF, Wallace Karia.
Pamoja na Manara kumuomba radhi Karia siku tatu baadaye na kuomba radhi hadharani kutokana na sintofahamu hiyo lakini kesi hiyo imeendelea kusikilizwa.
Soka Kesi ya Manara hadi Julai 20
Kesi ya Manara hadi Julai 20
Related posts
Read also