Na mwandishi wetu
Simba imepambana na Mashujaa FC kwa mbinde hadi kupata ushindi wa mabao 2-1 baada ya kuwa nyuma kwa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Ijumaa, Mei 2, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Mashujaa walipata bao la mapema katika dakika ta sita ya mchezo huo lililopachikwa wavuni na Jaffar Salum na kuiweka Simba katika wakati mgumu.
Simba ilianza kupambana kusaka bao la kusawazisha lakini juhudi zao hazikuweza kuzaa matunda kwa dakika zote 45 za mchezo huo licha ya kulisogelea mara kwa mara lango la Mashujaa.
Simba ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 65 lililofungwa na Leonel Ateba kwa mkwaju wa penalti kabla ya Ateba tena kufunga bao la pili kwa penalti katika dakika za nyongeza baada ya dakika 90 (90+14) za kawaida kumalizika.
Bao la pili la Simba lilipatikana wakati wapinzani wao Mashujaa wakiwa pungufu baada ya kipa wao, Patrick Mumthali kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 77.
Kwa kuwa Mashujaa walikuwa wamemaliza idadi ya wachezaji wa kufanyiwa mabadiliko, kiungo Abdulnasir Mohamed alilazimika kwenda kukaa golini na kufanikiwa kuwadhiti Simba kabla ya kuzamishwa na mkwaju wa penalti ya Ateba.
Simba ambao wamecheza mechi 23 hadi sasa wanaendelea kushika nafasi ya pili wakiwa na pointi 60 na hivyo kuzidiwa pointi 10 na mahasimu wao Yanga wanaoshika usukani wa ligi hiyo wakiwa wamecheza mechi 26.
Kwa upande wa Mashujaa wao wanabaki na pointi zao 30 katika mechi 27 walizocheza hadi sasa huku wakiendelea kushika nafasi yao ya 10.
Kimataifa Simba yailaza Mashujaa 2-1 kwa mbinde
Simba yailaza Mashujaa 2-1 kwa mbinde
Read also