Na mwandishi wetu
Simba imeendelea kula sahani moja na Azam FC katika mbio za kuisaka nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Geita Gold FC mabao 4-1 katika mechi iliyopigwa Jumanne hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo Simba imefikisha pointi 63 sawa na Azam, kila timu ikiwa imebakiwa na mechi mbili mkononi kabla ya pazia la ligi hiyo kufungwa rasmi.
Azam hata hivyo iko juu ya Simba kwa wastani mzuri wa mabao, timu zote hizo kila moja imefunga mabao 56 lakini Azam imefungwa mabao 20 wakati Simba imefungwa mabao 25.
Katika mchezo huo, Geita ndio waliokuwa wa kwanza kuliona lango la Simba katika dakika ya 11 kwa bao lililofungwa na kiungo Geofrey Julius ambaye alimalizia mpira uliomshinda kipa wa Simba.
Wakati timu hizo zikitarajiwa kwenda mapumziko, Geita wakiwa mbele, Simba ilipata bao la mkwaju wa penalti lililofungwa na Saido Ntibazonkiza, penalti iliyotolewa baada ya Shomari Kapombe kuchezewa rafu.
Dakika takriban 20 baada ya kuanza kipindi cha pili, Simba ilionesha uhai ikisukuma mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Geita ambao kipindi hicho hicho walipata pigo baada ya nahodha wao, Samwel Onditi kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Willy Onana.
Ni kama vile Simba ilineemeka baada ya Geita kubaki 10 uwanjani kwani dakika ya 73 iliandika bao la pili lililofungwa na Ntibazonkiza ambaye safari hii aliujaza wavuni kiufundi mpira uliotokana na adhabu ndogo iliyotolewa baada ya Onana kuchezewa rafu.
Simba haikuishia hapo, dakika ya 86, kazi kubwa iliyofanywa na Onana iliipa timu hiyo bao la tatu lililofungwa na Ladack Chasambi ambaye pia ndiye aliyeongoza bao la nne katika dakika tatu za nyongeza.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Azam iliichapa JKT Tanzania mabao 2-0, mabao ya washindi yakifungwa na Abdul Sopu na Feisal Salum, matokeo ambayo yameisaidia Azam kujiimarisha katika nafasi ya pili inayochuana na Simba.
Nayo Coastal Union iliichapa Kagera Sugar mabao 2-1, mabao ya washindi yakifungwa na Shedrack Mulungwe na Denis Modzaka wakati bao pekee la Kagera lilifungwa na Mbaraka Yusuph.
Soka Simba yaicharaza Geita 4-1
Simba yaicharaza Geita 4-1
Read also