Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Arne Slot amesema timu yake ina jukumu kubwa la kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) Jumapili hii kwa kuibwaga Tottenham Hotspur kwenye dimba la Anfield.
Sare ya Arsenal dhidi ya Crystal Palace Jumatano iliyopita inamaanisha Liverpool sasa inahitaji pointi moja tu ili kutangazwa mabingwa wa EPL msimu huu wa 2024-25 zikiwa zimebaki mechi nne kumalizika kwa ligi hiyo.
Mara ya mwisho Liverpool kubeba taji la EPL ilikuwa msimu wa 2019-20 wakati huo ikiwa chini ya kocha Jurgen Klop, taji ambalo lilipatikana wakati mashabiki hawaruhusiwi uwanjani kutokana na janga la Covid 19.
Ushindi huo ulikuwa tukio kubwa kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 kwa Liverpool kubeba taji hilo lakini haukufana kutokana na janga la Covid 19.
“Awali ya yote jukumu hilo ni kubwa kwa sababu tunafahamu mara ya mwisho klabu hii kubeba taji la ligi ilikuwa kipindi cha Covid, hivyo kwa sasa kila mtu anaiangalia mechi ya Jumapili lakini tunajua bado kuna kazi ya kufanya na kazi hiyo ni kupata walau pointi moja,” alisema Slot.
Slot alisema anaamini hata mashabiki wa Liverpool wanafahamu hilo na watawaunga mkono katika namna bora iwezekanavyo kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa kipindi chote cha msimu na wanafamu inahitajika pointi moja.
Spurs imekuwa na wakati mgumu kwenye Uwanja wa Anfield kwani tangu mwaka 2011 haikuwahi kupata ushindi kwenye uwanja huo lakini pia haina rekodi ya kuvutia kwenye ligi msimu huu.
Huu ni msimu wa kwanza kwa kocha Slot kuinoa Liverpool, kabla ya hapo alikuwa akiinoa Feyenoord ya Uholanzi, timu aliyoiacha akiwa ameiwezesha kubeba taji la Ligi Kuu Uholanzi.