Na mwandishi wetu
Simba imeitandika CS SFaxien ya Tunisia bao 1-0, ushindi ambao umetosha kuipa timu hiyo pointi tatu muhimu za kujiweka mguu sawa kuelekea robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ikiwa ugenini nchini Tunisia katika mechi iliyopigwa leo Jumapili, Januari 5, 2025, Simba imepata ushindi wa bao hilo pekee na hivyo kufikisha pointi tisa na kushika usukani katika Kundi A.
CS SFaxien kwa matokeo hayo wanashika mkia katika kundi hilo wakiwa na pointi moja wakati Bravos ya Angola inashika nafasi ya pili na CS Constantine ya Algeria inashika nafasi ya tatu zote zikiwa na pointi sita zikizidiana magoli.
Ahoua alifunga bao hilo dakika ya 33, bao lililotokana na mpira mrefu uliopigwa na Che Malone Fondoh na kumkuta Leonel Ateba aliyempasia Ahoua ambaye aliujaza wavuni kwa shuti maridadi la mguu wa kulia.
Simba waliendelea kulisakama lango la SFaxien na dakika tano baadaye, Ateba alimuunganishia pasi Elly Mpanzu ambaye shuti lake lilizaa kona ambayo haikuwa na madhara kwa SFaxien.
Kipindi cha pili kasi ya Simba iliendelea, dakika ya 59, Mpanzu aliambaa na mpira na kupiga krosi lakini beki mmoja wa SFaxien aliokoa kwa kichwa na kuzaa kona baada mpira huo kutoka nje ya lango la timu hiyo kwa juu.
Katika dakika 15 za mwisho, SFaxien wakicheza bila ya mashabiki wao uwanjani, waliongeza mashambulizi langoni mwa Simba kwa lengo la kusawazisha bao huku Simba wakihamia nyuma kulinda bao lao mpango ambao ulifanikiwa kwani hadi dakika 90 zinatimia matokeo yalibaki ya ushindi kwa Simba.
Kimataifa Simba yailaza CS SFaxien 1-0
Simba yailaza CS SFaxien 1-0
Read also