Na Hassan Kingu
Kama ambavyo mashabiki England wanalikumbuka bao la mkono alilowafunga Diego Maradona kwenye fainali za Kombe la Dunia 1986 ndivyo Ibrahim Bacca atakavyoendelea kukumbukwa kwa kufunga bao la mkono katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons.
Maradona mwenyewe alisema ule ulikuwa mkono wa ‘mungu’ na hadi anafariki dunia baadhi ya mashabiki England walimkumbuka kwa bao hilo haramu na wengine kusema kwamba amerudi kwenye mkono wa ‘mungu’ (back to the hand of god).
Katika fainali hizo za Kombe la Dunia zilizofanyika Mexico, Argentina walibeba kombe na baada ya hapo hadithi ya bao la mkono iliendelea kwa mashabiki England wakimuona Maradona kama mwanamichezo aliyeikosea heshima soka.
Mabao yote haramu, la Maradona haramu kama ilivyo la Bacca, kesho Yanga ikitwaa ubingwa kwa faida ya bao moja tutaipongeza kwa ubingwa lakini hapo hapo tutasema kuwa walibebwa na bao haramu.
Ni hivyo hivyo wakiwa wameshika nafasi ya pili na kukawa na uwakilishi kwenye michuano ya kimataifa, ikitokea wakawa na faida ya bao moja, tutasema bao haramu limeibeba Yanga.
Kukiwa na ushindani wa tuzo ya mfungaji bora ikatokea Bacca akapambana na kupata mabao kumzidi mpinzani wake kwa tofauti ya bao moja, pia tutasema bao haramu lambeba Bacca hadi kuwa mfungaji bora.
Yanga katika mechi hiyo iliwafunga Prisons 4-0, ushindi huu umesaidia kufifisha mjadala kwa kuwa hata ukiliondoa bao haramu bado Yanga imevuna pointi tatu muhimu na mabao 3-0.
Uharamu wa bao la Bacca hata hivyo upo wazi, haukwepeki hata kidogo licha ya ushindi mnono wa Yanga na Bacca kama mwanamichezo huenda anasikitika kwa kufunga bao haramu.
Ni kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry, huyu mwaka 2009 katika mechi dhidi ya Jamhuri ya Ireland alitumia mkono kuusogeza mpira uliozaa bao na kuiwezesha Ufaransa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2010.
Henry licha ya bao lake kuwa muhimu bado lilimtesa, alionekana akiwafariji wachezaji wa Jamhuri ya Ireland, kwa kauli yake alikuwa na nia ya kustaafu timu ya taifa kutokana na tukio hilo, alijiona ameukosea heshima mpira na huenda Bacca naye ni hivyo hivyo.
Kwenye mitandao ya kijami kumekuwa na picha inayomuonesha Lionel Messi naye akifunga bao kwa mkono kama kutetea bao la Bacca, hoja dhaifu, kosa la kwanza halihalalishi kosa la pili, yote hayo ni mabao haramu kwenye soka. Nini Messi hata Maradona naye alifunga bao haramu.
Mashabiki wanaweza wakalumbana wawezavyo asubuhi hadi jioni lakini hawawezi au watakuwa vichaa kusema bao la Bacca alilofunga kwa mkono si haramu eti kwa sababu tu Messi naye alifanya hivyo.
Uhalali/uharamu wa penalti ya Simba
Katika mjadala wa bao haramu la Bacca pia kumekuwa na mjadala mwingine kuhusu penalti iliyoipa Simba bao pekee dhidi ya JKT Tanzania, bao lililofungwa na Jean Ahoua.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Keifa Kayombo baada ya beki wa JKT, Mohammed Bakar kumshika beki wa Simba, Shomary Kapombe aliyekuwa akiuwahi mpira ulioelekezwa lango la JKT.
Kabla ya kujadili uhalali au uharamu wa penalti ile, tutajaribu kufikiri ingekuwaje kama mwamuzi huyo asingepuliza filimbi. Bila shaka angeonekana mwamuzi wa ajabu na asiyejua sheria ndogo na ya kawaida katika soka.
Kuna hoja ambayo imeibuka, hoja yenyewe ni kukiri kwamba kosa lilifanyika lakini Kapombe alijipeleka chini kumshawishi mwamuzi kwamba alifanyiwa dhambi lakini alikuza tukio, dhambi ndogo aliifanya kubwa.
Hili linaweza kuwa jambo la kweli lakini ni vipi mwamuzi angeweza kung’amua kwamba Kapombe alikuza tukio la kushikwa na beki kwamba Kapombe angeweza kuweweseka na si kuanguka kama ilivyotokea.
Kimsingi tukio au kosa la Kapombe kushikwa lilifanyika na sote tuliliona na mwamuzi alitakiwa kupuliza filimbi, asingepuliza tungemshangaa, sasa kashikwa kiasi gani na ni kwa nini hakuweweseka badala yake akaanguka, hilo ni suala jingine gumu.
Kibinadamu kuna baadhi ya mambo ni magumu mno kuyang’amua na hivyo la msingi ni kwa wachezaji hasa mabeki kuwa makini na makosa wanayoyafanya hasa kwenye maeneo ya hatari.
Nasema hivyo kwa sababu washambuliaji walio wengi unapomchezea rafu katika eneo hilo anajitahidi kulikuza kwa kumshawishi mwamuzi na mwamuzi si malaika kujua ukubwa wa tukio na uimara wa mfanyiwa tukio kama linaweza kumuangusha au la.
Kapombe huyu huyu naamini angekuwa ameshikwa na kibaka asingeanguka, angekimbia au angekuwa anakimbilia dhahabu yeye na beki wa JKT, pia asingeanguka angeongeza kasi kuiwahi dhahabu.
Ni hivyo hivyo kwa washambuliaji walio wengi ukimgusa kidogo tu eneo la penalti anatumia kosa hilo kupata faida ya penalti na mwamuzi hawezi kuona tukio la beki kumkwatua mshambuliaji akaliacha.
Washambuliaji wengi inaweza kuwa zaidi ya asilimia 90 wanapokwatuliwa kidogo kwenye eneo la penalti hata kama ni tukio la kumfanya ayumbe kidogo na kuendelea kuuwahi mpira hawafanyi hivyo.
Kwa mshambuliaji tukio hilo kwake hulifanya kuwa faida na mwamuzi akijiridhisha mchezaji kakwatuliwa suala la ukubwa wa ukwatuaji ni gumu kulipima, anachoweza kufanya ni kupuliza filimbi kwa sababu kosa limefanyika.
Mpira unapokuwa kwenye kasi kuna makosa ambayo mchezaji hasa mabeki huyafanya bila kujijua, kama vile kumshika mchezaji na ndio maana baadhi yao hujirudi hapo hapo na kuonesha ishara ya mikono kuwa mbali.
Lengo la kufanya hivyo ni kumshawishi mwamuzi asiwaadhibu lakini wakati huo tayari mfanyiwa kosa ameshakwenda chini na mwamuzi ameshaona na kuchukua hatua, na hatua hutegemea na eneo husika la tukio.
Katika mazingira ya matukio ya aina hii tutajadili na kujadili kadri yatakavyokuwa yakitokea lakini mwishowe tutakubali kwamba dhambi imefanyika na ukubwa wa dhambi ataachiwa mwamuzi aamue.