Na mwandishi wetu
Hatimaye nyota imeanza kung’aa kwa mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube baada ya kufunga mabao matatu wakati timu yake ikiilaza Mashujaa FC mabao 3-2 katika Ligi Kuu NBC.
Mabao hayo matatu au hat trick aliyoyafunga kwenye dimba la KMC leo Alhamisi ni ya kwanza kwa Dube katika ligi msimu huu na hivyo anakuwa kama anafungua akaunti ya mabao.
Dube amekuwa akiandamwa na ukame wa mabao msimu huu hali ambayo iliibua malalamiko kwa baadhi ya mashabiki hadi kuibuka hoja kwamba Yanga ilikosea kumsajili kutoka Azam FC.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 30 kwenye ligi wakati Dube anakuwa amefunga mabao matatu ya ligi hiyo na kukabidhiwa mpira lakini pia ametajwa kuwa nyota wa mchezo huo.
Dube alianza kuandika bao la kwanza mapema dakika ya saba kwa shuti la chinichini akiunganisha mpira ulioanzia kwa Stephane Aziz Ki aliyempasia Pacome Zouzoua kabla ya mpira kumkuta mfungaji.
Mashujaa hata hivyo walionekana kupambana kutaka kusawazisha bao hilo na katika dakika ya 33 walifanya shambulizi kali ambapo ushirikiano wa Ismail Mgunda na David Uromi nusura uipe timu hiyo bao.
Dube aliwakatisha tamaa Mashujaa dakika ya 21 alipounganisha kwa kichwa krosi iliyoanzia kwa Pacome na mpira kumbabatiza Clement Mzize na beki wa Mashujaa waliokuwa wakipambana kabla ya kumkuta mfungaji.
Juhudi za Mashujaa zilizaa matunda dakika ya 45 baada ya Uromi kuufumania mpira na kufumua shuti la chinichini na mpira kumshinda kipa Aboubakar Khomein ambaye alijichanganya wakati akitaka kuudaka.
Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kasi lakini walikuwa ni Yanga waliopata bao la tatu dakika ya 52 mfungaji akiwa Dube safari hii akifunga tena kwa kichwa.
Dakika takriban 10 baada ya kuingia kwa bao hilo, Mashujaa walijibu mapigo kwa kuandika bao la pili lililofungwa na Idris Stambuli kwa shuti lililomshinda Khomein.
Mashujaa waliendelea na dhamira yao ya kutaka bao la kusawazisha na kuonesha wakati wote dhamira yao katika jambo hilo licha ya Yanga kufanya mabadiliko kadhaa ikiwamo kumtoa Mzize na kumuingiza Mudathir Yahya na baadaye Duke Abuya na nafasi yake kuingia Salum Aboubakar ‘Sure Boy’.
Kwa upande wa Mashujaa nao waliwatoa Balama na kumuingiza Josephat, baadaye Mginda na kumuingiza Nushi na Uromi ambaye nafasi yake aliingia Mundhir.
Mabadiliko hayo kwa ujumla wake hayakuwayumbisha Mashujaa badala yake waliendelea kuwa wapambanaji kwa muda wote wa mchezo ingawa mwisho wa mchezo matokeo hayakuwa mazuri kwao.
Kimataifa Dube atupia matatu Yanga ikiwaliza Mashujaa
Dube atupia matatu Yanga ikiwaliza Mashujaa
Read also