Marseille, Ufaransa
Timu ya soka ya wanawake ya Brazil itaumana na Marekani katika mechi ya fainali ya Michezo ya Olimpiki baada ya kuichapa Hispania mabao 4-2 katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa Jumanne hii.
Brazil ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya sita ambalo lilitokana na makosa ya Iene Peredes wa Hispania aliyejifunga.
Muda mchache kabla ya timu kwenda mapumziko, Brazil iliongeza bao la pili lililofungwa na Gabi Portilho na kuingia kipindi cha pili na nguvu mpya zilizozaa bao la tatu lililofungwa na Adriana dakika ya 71.
Hispania ilipambana na hatimaye kuneemeka na bao la kujifunga la Duda Sampaio dakika ya 81 lakini ilijikuta ikichapwa bao la nne lililofungwa na Kerolin katika dakika za lala salama.
Bao hilo hata hivyo halikuwarudisha nyuma Hispania ambao katika dakika hizo hizo nao walifanikiwa kupata bao la pili mfungaji akiwa ni Salma Paralluelo.
Mshindi kati ya Brazil na Marekani ambao wataumana Jumamosi mjini Paris atabeba medali ya dhahabu wakati Ijumaa Hispania itacheza mechi ya kuwania medali ya shaba dhidi ya Ujerumani.
Mechi ya Brazil na Marekani inawakumbusha Brazil matukio mawili ya timu hizo kukutana katika hatua ya fainali kwenye Michezo ya Olimpiki 2004 Athens na 2008 Beijing ambapo mara zote Brazil ilishindwa kutamba.
Ushindi wa Brazil pia utampa nafasi nyota wao mkongwe Marta, 38, kucheza mechi ya fainali baada ya kupewa adhabu ya kukosa mechi mbili ambayo ameimaliza kwa kukosa mechi za robo na nusu fainali.
Marta ambaye anashikilia rekodi ya kuiwakilisha Brazil katika Michezo ya Olimpiki mara sita, amesema kwamba hii itakuwa mara yake ya mwisho kuiwakilisha timu ya taifa ya Brazil kwenye Olimpiki.
Kimataifa Brazil yafuzu fainali Olimpiki 2024
Brazil yafuzu fainali Olimpiki 2024
Read also