
Bloemfontein, Afrika Kusini
Timu ya Yanga, leo Jumapili imeibamiza Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mabao 4-0 katika mechi ya Kombe la Toyota iliyopigwa kwenye dimba la Toyota, Bloemfontein, Afrika Kusini na kubeba taji hilo.
Prince Dube alikuwa wa kwanza kuliona lango la Chiefs dakika ya 25 kwa bao lililotokana na pasi ndefu ya Maxi Nzengeli na mpira kumkuta Khalid Aucho ambaye kwanza alishindwa kuumiliki vizuri lakini alifanikiwa kumsogezea Dube aliyeujaza wavuni.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana na dakika ya 31, Yao alimuunganishia pasi Mzize ambaye naye alimpasia Maxi lakini akiwa katika nafasi nzuri, Maxi alishindwa kuumiliki vizuri mpira na kupiga shuti lililokosa umakini.
Chiefs wanaonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasredine Nabi, walijibu mapigo dakika ya 42 kwa Mfundo Kilakazi aliyeinasa vizuri pasi ya kisigino na kujigeuza haraka kabla ya kufumua shuti la mguu wa kushoto ambalo hata hivyo kipa wa Yanga, Djigui Diarra alilidaka kwa ulaini.
Muda mfupi kabla ya mapumziko, Stephane Aziz Ki aliipatia Yanga bao la pili akiyatumia makosa ya beki wa Chiefs, Nkosana Mbutu na mpira kumkuta Dube aliyemsogezea Duke Abuya kabla ya kumkuta Aziz Ki aliyeujaza wavuni.
Dakika 10 baada ya mapumziko, Yanga waliandika bao la tatu lililofungwa na Clement Mzize kwa mpira ulioanzia kwa Maxi ambaye alipiga pasi ndefu na kumkuta Dube aliyemsogezea mfungaji.
Yanga iliandika bao la nne dakika ya 63 mfungaji akiwa Aziz Ki ambaye kabla ya kufunga bao hilo alimhadaa beki mmoja wa Chiefs na kuujaza mpira wavuni kwa mguu wa kulia ambao si mguu anaopenda kuutumia.

Katika mechi hiyo, Yanga chini ya kocha Miguel Gamondi pia ilionesha upana wa kikosi chake kwa kuwatoa, Khalid Aucho, Dube na Abuya na kuwaingiza Mudathir Yahya, Pacome Zouazoua na Aziz Andambwile.
Yanga pia katika mabadiliko mengine iliwatoa Aziz Ki, Mzize na Dickson Job na nafasi zao kuingia Clatous Chama, Jean Baleke na Bakari Mwamnyeto.
Wakati huo huo mfungaji wa mabao mawili ya Yanga, Aziz Ki ia ameibuka nyota wa mchezo huo au man of the match na kuzawadiwa hundi ya Randi 5000 za Afrika Kusini.
Hiyo ni mechi ya tatu kwa Yanga ambayo ipo Afrika Kusini ikijinoa kwa msimu mpya wa 2024-25, ilianza kwa kufungwa 2-1 na Augsburg FC ya Ujerumani na baada ya hapo ikailaza TS Galaxy ya Afrika Kusini bao 1-0.