Los Angeles, Marekani
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Vinícius Júnior hajafurahishwa na kiwango cha soka la Brazil kwenye fainali zinazoendelea za Copa America ingawa amesema wanaweza kuboresha kiwango hicho.
Kauli hiyo ya Vinicius Jr imekuja baada ya timu hiyo kuanza mechi yao ya kwanza ya fainali za Copa America ya Kundi D kwa sare ya bila kufungana na Costa Rica jana Jumatatu mjini Los Angeles.
Ikiongozwa na safu ya ushambulijai iliyokuwa na washambuliaji wawili mahiri wa Real Madrid Vinicius Jr na mwenzake Rodrygo, Brazil ilipiga mashuti 19 langoni mwa Costa Rica lakini kati ya hayo ni matatu tu yaliyolenga goli.
“Tunajua tunaweza kuboresha soka letu, ni lazima tuwe katika ubora, pia mimi nafahamu nini cha kuboresha na nini cha kufanya kwa ajili ya timu yetu,” alisema Vinicius Jr.
Brazil au Selecao ilipata tabu kuupenya ukuta wa Costa Rica ulioongozwa na mabeki watano hadi kocha wa timu hiyo Dorival Junior kuamua kumtoa Vinícius Jr dakika ya 71 na kumuingiza Endrick.
“Tulijaribu kumtumia Vinicius kwenye winga lakini hatukufanikiwa, baadaye tukamuweka kati lakini bado hatukuweza kupenya, alikabwa vizuri,” alisema Dorival.
Dorival pia alimtoa Raphinha katika dakika ya 71 na kumuingiza Sávio lakini bado timu yake ilipata wakati mgumu kuipenya Costa Rica ingawa alisema ilikuwa lazima kusaka suluhisho na ndio maana alilazimika kufanya mabadiliko.
“Kocha mpya, wachezaji wapya, kila kitu kinahitaji muda, mashabiki wetu wanataka kila kitu kwa haraka lakini tunakwenda kidogo kidogo, mechi ijayo nina hakika tutacheza vizuri zaidi kwa sababu tayari tunaelewa mashindano haya yalivyo,” alisema Vinicius.