Munich, Ujerumani
Fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024 zinaanza leo Ijumaa kwenye dimba la Allianz Arena mjini Munich, Ujerumani, swali ni je nani atalibeba taji hilo linaloshikiliwa na Italia?
Mechi 51 zitakazoshirikisha timu 24 zitapigwa kwa muda wa siku 31 kuanzia leo hapo Allianz Arena na kuhitimishwa Julai 14 kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Berlin ambapo bingwa atapatikana.
Je ni mabingwa watetezi Italia watakaobeba taji, vipi kuhusu wenyeji Ujerumani, na je vipi kuhusu England ambao nao wanatajwa kwa nguvu na kwa matumaini makubwa ya kulibeba taji hilo?
Mafanikio hadi kubeba taji la Euro 2024 yanaanzia hatua ya makundi, wenyeji Ujerumani walio Kundi A atafungua pazia la fainali hizo kwa kuumana na Scotland katika kundi ambalo pia lina timu za Hungary na Switzerland.
Ujerumani ambayo wachambuzi wengi hawaamini kama wana timu nzuri ya kutoa ushindani, ni kama ilivyokuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 lakini timu hiyo bado inapewa nafasi kubwa ya kuwa kinara wa Kundi A japo haifikiriwi kwa sana katika timu zinazoweza kubeba taji.
Baada ya Ujerumani timu nyingine inayopewa nafasi ya kusonga mbele katika kundi hilo ni Scotland ingawa bado huwezi kuzibeza Hungary na Switzerland katika mbio za kutoishia hatua ya makundi.
Kazi kubwa ipo Kundi B lenye timu za Hispania, Croatia, Italia na Albania, bingwa mtetezi Italia ana nafasi kubwa ya kusonga mbele pamoja na Croatia lakini bado Hispania nayo heshima yake katika soka ipo pale pale na hakuna atakayeshangaa ikiongoza au kushika nafasi ya pili katika kundi hilo.
Croatia, Italia na hata Hispania ni timu ambazo unaweza pia kuziweka katika timu zenye uwezo wa kubeba taji, kwao mafanikio si kuvuka hatua ya makundi pekee.
Kwenye Kundi C, England imeendelea kupewa nafasi kubwa ya kushika usukani wa kundi hilo na kusonga mbele ikisubiri kuungana na Denmark, Serbia au Slovenia.
England itatupa karata yake ya kwanza Juni 16 dhidi ya Denmark wakati Slovenia itaikabili Serbia siku hiyo hiyo, pamoja na England kupewa nafasi kubwa lakini mechi hizo za kwanza pia zitatoa picha ya mwelekeo wa timu hizo.
Katika mechi yake ya mwisho ya kujipima nguvu, England haikuwa na matokeo mazuri mbele ya Iceland lakini timu hiyo ilijifariji kwa kuitaja mechi hiyo kama tukio la kuwaamsha na kuwataka wawe imara kwenye fainali za Euro 2024.
Kwa hiyo kinachosubiriwa ni hiyo Jumapili kuona England itaanzaje fainali hizo huku ikiweka kando majigambo na matumaini makubwa ambayo imekuwa ikipewa kupitia vyombo vya habari.
Katika kundi hili, England ni timu pekee ambayo imekuwa ikitajwa kuwa bora na imara na kwamba ina uwezo wa kubeba taji.
Kundi D nalo lina ugumu wake nguvu ya Ufaransa katika soka la dunia bado si ya kubeza hasa inapokumbukwa ilipofikia hatua ya fainali za Kombe la Dunia 2022.
Katika kundi hili Ufaransa inapewa nafasi kubwa ya kushika usukani na kusonga mbele, baada ya Ufaransa timu nyingine ni Uholanzi nayo si haba ina jina kubwa na imebeba matumaini ingawa Austria na Poland zina nafasi ya kufanya maajabu.
Austria hasa katika miaka ya karibuni imeweza kuonesha ubora ambao wachambuzi wengi wamekuwa wakisubiri kuushuhudia kwenye michuano mikubwa ikiwamo hii ya Euro 2024.
Ni Ufaransa pekee katika kundi hili ambayo unaweza kabisa kuitaja kuwa timu yenye sifa zote za kubeba taji hilo.
Kundi E lenye timu za Ubelgiji, Slovakia, Romania na Ukraine limeonekana kuwapa wakati mgumu wachambuzi wengi wa soka kujua nani na nani wataongoza kundi, ni kundi ambalo unaweza kusema tusubiri kitakachojiri kwenye mechi za makundi.
Kundi F ambalo ni kundi la mwisho kwenye orodha ya timu 24 shiriki za Euro 2024 lina timu za Uturuki, Ureno, Georgia na Jamhuri ya Czech.
Ureno imekuwa chaguo lililobeba matumaini ya wengi katika kundi hilo, timu yenye mkongwe Cristiano Ronaldo haitajwi kuishia hatua ya makundi tu bali inatajwa pia katika timu zenye uwezo wa kulibeba taji.
Baada ya Ureno katika kundi hili kuna ugumu kidogo katika kuzichambua timu zilizobaki na kujua nani ni zaidi ya nani na ambaye atakuwa nyuma ya Ureno ingawa jina la Uturuki linaonekana kuchomoza zaidi.
Kimataifa Nani kubeba taji Euro 2024?
Nani kubeba taji Euro 2024?
Read also