Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves amefikishwa mahakamani na kukana kumbaka msichana katika klabu moja ya usiku ya mjini Barcelona.
Alves, 40, amekuwa mahabusu tangu alipokamatwa mara ya kwanza Januari mwaka jana akituhumiwa kumbaka msichana mmoja wakati akifurahia maisha na wenzake katika klabu hiyo ya usiku.
Waendesha mashtaka katika hoja zao wanaitaka mahakama hiyo impe Alves kifungo cha miaka tisa jela pamoja na malipo ya fidia kwa msichana anayedaiwa kufanyiwa ubakaji huo.
Msichana anayedaiwa kubakwa na mchezaji huyo alisema wakiwa katika klabu ya usiku, mchezaji huyo alimdanganya na kumuingiza chooni katika eneo la watu maarufu kabla ya kumlazimisha kufanya naye ngono.
Katika utetezi wake Alves alisema msichana huyo angeweza kuondoka kwani hakukuwa na ulazima wa kuendelea kuwa eneo hilo na akaongeza kuwa msichana huyo hakuwahi kumwambia aachane naye.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Alves akiwa na rafiki yake, aliwanunulia mvinyo wasichana watatu na baadaye akamuomba mmoja wao amsindikize eneo jingine ambalo lilikuwa na choo lakini msichana huyo alikuwa hajui.
Walieleza kwamba baada ya kuingia ndani, Alves alianza kuonesha ubabe na kumlazimisha msichana huyo kufanya naye ngono licha ya msichana huyo kulalamika akitaka Alves amuachie.
Awali, Alves aliwahi kukiri kumjua msichana huyo lakini alisema hakufanya lolote baya ingawa baadaye alisema kwamba kama kuna kitu kilichofanyika basi kulikuwa na makubaliano.
Alves pia katika utetezi wake wa hivi karibuni alinukuliwa akidai kwamba siku ya tukio analodaiwa kulifanya alikuwa amelewa na kwamba anachodaiwa kukifanya kilitokana na ushawishi wa ulevi.
Mara baada ya kuhusishwa na kashfa hiyo klabu aliyokuwa akiichezea ya Pumas UNAM ya nchini Mexico, Januari mwaka jana ilitangaza kuvunja mkataba na mchezaji huyo.
Kimataifa Dani Alves akana kubaka
Dani Alves akana kubaka
Read also