Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limemteua Mwenyekiti wa Shirikisho cha Klabu Afrika (ACA) na Rais wa Yanga, Hersi Saidi kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi za Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan).
Hayo yameelezwa Jumamosi hii na Rais wa TFF, Wallace Karia katika mkutano mkuu wa mwaka wa shirikisho hilo unaofanyika mjini Iringa.
Karia alisema kuwa Hersi ameteuliwa kuingia katika kamati hiyo kwa vile ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, nafasi aliyoipata baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa ACA takribani wiki mbili zilizopita.
“Kwa nafasi ya kuwa rais wa klabu Afrika, Hersi Saidi ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na hivyo ameingia kwenye Kamati ya Maandalizi ya Chan na Afcon,” alisema Karia.
Hersi aliingia madarakani Yanga akirithi mikoba ya Dk Mshindo Msolla, ambapo katika uongozi wake amefanikiwa kuibadilisha timu hiyo kucheza soka la kisasa na ushindani wa hali ya juu huku ikiendelea kusajili wachezaji wenye viwango vya juu Afrika.