Rio de Janeiro, Brazil
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetangaza kufanya uchunguzi baada ya kutokea vurugu katika mechi kati ya Brazil na Argentina na kusababisha mechi hiyo kuchelewa kuanza kwa nusu saa.
Mechi hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyopigwa Jumanne kwenye Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro ilichelewa kuanza baada ya kutokea vurugu zilizosababisha polisi watumie virungu kuwatuliza mashabiki wa Argentina.
Mara tu baada ya kuanza kwa vurugu, nahodha wa Argentina Lionel Mess aliwaongoza wachezaji wake kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na baadaye alinukuliwa akisema kwamba alilazimika kufanya hivyo kwa sababu alihofia hali ingeweza kuwa mbaya zaidi.
Messi aliwalaumu polisi ambao walitumia virungu kuwakabili mashabiki hao ambao nao walivunja viti na kuvitumia kujihami wakati wengine walikimbilia katikati ya uwanja ambapo baadaye shabiki mmoja alionekana akiwa amebebwa kwenye machela na watu wa huduma ya kwanza.
Katika sakata hilo ambalo lilianza wakati nyimbo za taifa zikiimbwa, huenda vyama vya soka vya Brazil na Argentina vyote vikajikuta vikikumbana na adhabu ya Fifa.
Wakati vurugu zikiendelea, wachezaji wa timu zote walionekana kuwafuata mashabiki wao na kuanza kuwatuliza ambapo kipa wa Argentina na klabu ya Aston Villa, Emiliano Martinez alionekana akijaribu kumnyang’anya polisi mmoja kirungu.
“Fifa inathibitisha kwamba kamati ya nidhamu imeanza uchunguzi dhidi ya Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) na Chama cha Soka Argentina (AFA),” ilieleza taarifa ya Fifa iliyopatikana Ijumaa.
Adhabu inayoweza kutolewa kwa kosa hilo ni faini au uwanja kufungiwa, Brazil inahusishwa na kosa la kushindwa kutuliza amani kwenye mechi wakati Argentina inahusishwa na kosa la vurugu za mashabiki.
Baadaye mechi hiyo iliendelea na kuchezwa kwa dakika 90 kama kawaida na Argentina ambao ndio mabingwa wa dunia, walitoka na ushindi wa bao 1-0.