Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Barcelona, Lamine Yamal, 16, amevunja rekodi kwa kufunga bao katika Ligi Kuu Hispania au La Liga akiwa na umri mdogo baada ya timu yake kutoka sare ya mabao 2-2 na Granada.
Yamal (pichani) amefunga bao hilo jana Jumapili akiwa na miaka 16 na siku 87 na kuweka rekodi mpya huku akivunja rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na Fabrice Olinga tangu mwaka 2012 ambaye akiwa Malaga aliifungia timu hiyo bao akiwa na miaka 16 na siku 98.
Wachezaji wanaofuata kwa kufunga mabao katika ligi hiyo wakiwa wanakamilisha tano bora ni Iker Munian, Ansu Fati na Xisco Nadal ambao nao walifunga mabao kabla ya kufikisha miaka 17.
Bao la Yamal lilikuja wakati mzuri kwani katika mechi hiyo, Barca ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Granada, timu ambayo haikupewa nafasi yoyote ya kuisumbua Barca.
Yamal hata hivyo hakudumu katika mechi hiyo, alitolewa dakika ya 76 baada ya kuomba na baadaye kocha wake Xavi alisema mchezaji huyo yuko salama ingawa atafuatiliwa kwa karibu katika siku chache zijazo.
Yamal pia ana rekodi ya kuichezea na kuifungia goli Hispania, alifanya hivyo Septemba 8 katika mechi dhidi ya Georgia, mechi ambayo Hispania ilishinda kwa mabao 7-1 na kuvunja rekodi iliyowekwa na nyota mwenzake wa zamanI wa Barca, Gavi aliyeichezea timu hiyo akiwa na miaka 17 na siku 62 mwaka 2021.
Kimataifa Bao la Yamal lavunja rekodi La Liga
Bao la Yamal lavunja rekodi La Liga
Read also