Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amepanga kukiboresha kikosi chake kwa kusajili wachezaji wapya watakaoiongezea nguvu timu hiyo katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo amebainisha kuwa ili kulikamilisha suala hilo mapema, amepanga kukutana na uongozi wa timu hiyo ili kuzungumzia suala hilo na kuona watafanikiwa vipi katika mipango yao.
“Hatua tuliyopo ni ngumu, tunapaswa kuwa na kikosi imara kitakachokwenda kushindana siyo kushiriki ndio maana nataka kuongeza wachezaji watatu au wawili kwenye dirisha dogo ili kumudu ushindani uliopo huko,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alitaja nafasi ambazo anataka kuziboresha kuwa ni ushambuliaji, winga pamoja na beki mmoja wa kati, lengo likiwa ni kuongeza ushindani kwa wachezaji waliopo kwenye maeneo hayo.
Gamondi alisema malengo yake ni kuvuka hatua hiyo ya makundi hivyo ili kutimiza lengo hilo lazima wawe na timu iliyokamilika na kuhimili ugumu na ushindani uliopo kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika.
Kocha huyo alieleza kuwa anajivunia kikosi chake ambacho kimemfikisha hapo lakini kutokana na ugumu wa huko wanakokwenda lazima kuongeza nguvu ili wawe na uhakika wa kupata kile wanachokikusudia.
Yanga imetinga hatua hiyo ikiwa imepita miaka 25 tangu mara ya mwisho ilipofika hatua hiyo baada ya kuisukuma nje Al Merrikh ya Sudan kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0. Mechi ya kwanza Yanga ilishinda mabao 2-0 ugenini kabla ya kushinda bao 1-0 nyumbani.