London, England
Mwenyekiti wa klabu ya West Ham, David Sullivan ameamua kumuaga kiaina nahodha wao, Declan Rice baada ya kusema ana uhakika asilimia 99 mchezaji huyo ataondoka katika klabu hiyo.
Sullivan alitoa kauli hiyo mara baada ya timu hiyo kubeba taji la Europa Conference Ligi kwa kuichapa Fiorentina mabao 2-1 na kuweka historia kwa kubeba taji la kwanza kubwa baada ya miaka 43.
Rice (pichani) katika siku za karibuni amekuwa akitajwa kuwindwa na klabu za barani Ulaya lakini Sullivan alisema walimpa ahadi kwamba akijitoa kwa hali na mali kwa timu hiyo watampa nafasi ya kuondoka.
“Tulimpa ahadi, majira ya kiangazi msimu uliopita kwamba akiweza kutupa kila kitu tutamruhusu aondoke katika klabu, hivyo kwa sasa ni jambo la haki na sahihi kulifanya,” alisema Sullivan.
Juzi Jumatano Rice alikuwa nahodha wa tatu katika historia ya klabu hiyo kubeba taji la klabu hiyo akifuata nyayo za watangulizi wake Bobby Moore aliyebeba taji la Washindi Ulaya mwaka 1965 na Billy Bonds aliyebeba taji la FA mwaka 1975 na 1980.
Tangu atue kikosi cha kwanza cha West Ham msimu wa 2016-17 akitokea katika akademi ya klabu hiyo, Rice ameichezea timu hiyo mara 245 na kufunga mabao 15 huku akionyesha uwezo katika nafasi ya kiungo.
Awali aliiwakilisha timu ya Jamhuri ya Ireland mara tatu kabla ya kubadili na kuanza kuichezea timu ya England na hadi sasa ameichezea timu hiyo mara 41 na alicheza mechi tano za England kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar.
Katika mkataba wake na West Ham, Rice amebakisha mwaka mmoja lakini kinachosubiriwa sasa ni kujua timu anayoelekea huku Arsenal ikitajwa kuwa moja ya timu zinazovutiwa na mchezaji huyo.
Rice ambaye ametangazwa kuwa mwanasoka bora wa mwaka wa Uefa Conference Ligi, amejijengea umaarufu kwa kucheza soka la kuvutia katika eneo la kiungo kwa namna anavyojua kuusoma mchezo na kutopoteza mipira.