Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Lionel Messi ameagwa rasmi na timu hiyo kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Clemnont Foot, mechi ambayo PSG ililala kwa mabao 3-2 huku mshabiki wakimzomea mchezaji huyo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii kwenye dimba la Parc des Princes, Messi alijikuta akizomewa na baadhi ya mashabiki mara baada ya jina lake kutajwa.
PSG ilitangaza jina la mchezaji huyo kabla ya mechi na kuthibitisha kwamba hatoongeza mkataba wake wa sasa wa miaka miwili ambao umefikia ukomo na mechi dhidi ya Clemnont ilikuwa fursa kwake kuwaaga rasmi mashabiki.
Hata hivyo zomea hiyo haikuwa ya muda mrefu kwani dakika chache baadaye Messi aliingia uwanjani na watoto wake watatuo akiwa amewashika huku akionekana mwenye tabasamu na kabla ya kupiga picha ya timu, aliwabusu kila mmoja kwenye bapa la uso.
Messi pia wakati wa mechi alizomewa alipokosa bao ambalo lingeweza kufanya matokeo yawe sare ya 3-3 alipounganishiwa pasi na Kylian Mbappe lakini akiwa karibu na kipa akapiga shuti lililopaa juu.
Hata hivyo katika kilichoonekana kutosumbuliwa na zomea iliyotoka kwa sehemu ndogo ya mashabiki, Messi alitoa shukrani kwa ujumla na kuitakia yaliyo mema klabu hiyo ya jijini Paris.
“Ningependa kuishukuru klabu, jiji la Paris na watu wake kwa miaka miwili niliyokuwa hapa, nawatakia kila lenye heri kwa mambo yao baadaye,” alisema Messi.
Messi pia aliwahi kuzomewa katika moja ya mechi baada ya kusimamishwa na klabu kwa wiki mbili alipoenda Saudi Arabia bila ruhusa ingawa baadaye alisamehewa na ndipo alipokutana na zomea hiyo katika mechi aliyocheza baada ya kufutiwa adhabu.
Katika miaka yake miwili PSG, Messi ameiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1 mara mbili pamoja na taji la Ufaransa, amefunga mabao 32 na ametoa asisti 35 katika michuano yote.