London, England
Man City imepiga hatua nyingine muhimu katika azma yake ya kubeba mataji matatu msimu huu baada ya kuibwaga Man United kwa mabao 2-1 katika mechi ya fainali ya Kombe la FA na kubeba taji hilo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii kwenye dimba la Wembley, Man City ilipata ushindi huo kwa mabao ya nahodha Ilkay Gundogan katika dakika ya kwanza na ya 51, yote yakitokana kazi nzuri ya Kevin De Bruyne wakati bao pekee la United likifungwa kwa penalti na Bruno Fernandes katika dakika ya 33.
Man City tayari ina mataji mawili baada ya kubeba lile la Ligi Kuu England (EPL) na sasa inasubiri Juni 10 itakapoumana na Inter Milan katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Iwapo Man City itaibwaga Inter katika fainali hiyo itakayopigwa mjini Istanbul, Uturuki itakuwa imeweka rekodi ambayo mara ya mwisho kwa England iliwekwa na Man United mwaka 1999 ilipobeba mataji matatu yaani EPL, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Gundogan ambaye hivi karibuni kocha wake Pep Guardiola ameelezea umuhimu wake ndani ya kikosi cha Man City, aliweka rekodi kwa kufunga bao la mapema katika Kombe la FA akiwa amefunga katika sekunde ya 12.
Bao hilo linamfanya awe ameipiku rekodi ya Luois Saaha ambaye mwaka 2009 akiwa mchezaji wa Everton alifunga bao la mapema katika sekunde ya 25 katika mechi dhidi ya Chelsea.
Kwa majirani zao katika jiji la Manchester, Man United, matarajio yao ya kubeba taji la pili msimu huu yametoka kapa na sasa wanabaki na taji moja tu la Carabao ambalo ni la kwanza katika kipindi cha miaka sita.
Kocha Erik ten Hag bila shaka atakuwa na kazi nzito ya kufanya msimu ujao hasa baada ya kuonyesha matumaini makubwa msimu huu akifanikiwa kuingia top four na msimu ujao atashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mipango ya msimu ujao ya Man United, jina la kiungo wa Chelsea, Mason Mount limo kwenye mpango wa Ten Hag na haitashangaza akiichezea timu hiyo msimu ujao kama ilivyo kwa mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane ambaye pia yumo kwenye hesabu za Ten Hag kwa ajili ya msimu ujao.
Kimataifa Man City yabeba taji FA
Man City yabeba taji FA
Read also