Na mwandishi wetu
Wawakilishi wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga SC imeeleza kuwa kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya mechi ya kesho Jumapili kuhakikisha wanapata matokeo dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
Yanga itashuka ugenini kwenye Uwanja wa Godswill, Uyo kuvaana na Rivers kwenye mechi ya kwanza ya robo fainali ya michuano hiyo itakayopigwa kuanzia saa 10.00 jioni.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema tangu wamefika juzi nchini Nigeria hali ya hewa imekuwa rafiki kwao na wachezaji wote wamekuwa wakijifua kwa umakini mkubwa kwa ajili ya kupata matokeo mazuri ugenini.
“Kitu cha kwanza hali ya hewa ni nzuri, tumefanya mazoezi ya kujiweka sawa na kimbinu pia, tumetengeneza mikakati yetu namna ya kushambulia na niseme tumemaliza kuweka sawa mipango tuliyonayo kuelekea mechi hiyo.
“Kikubwa hii ni mechi ya kuingia nusu fainali, ni mechi mbili za dakika 180 na wachezaji wako makini na hakuna mchezaji ambaye ana mashaka, kila mtu anaonesha uwanjani kama amehamasika kwenye mechi hii na ya marudiano,” alisema Kaze.
Alisema kikosi hicho bado kimeumia na matokeo ya mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu NBC kwa kufungwa mabao 2-0 na Simba, hivyo wanataka kuutumia mchezo dhidi ya Rivers kujipooza na kuonesha kuwa matokeo yaliyopita yalikuwa kama ajali kwao.
Kuelekea mechi hiyo, Yanga pia inataka kulipa kisasi kwa Rivers kwa kufungwa na kufurushwa kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikikubali kipigo cha bao 1-0 katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.
Timu hizo zinakutana kwenye hatua hiyo baada ya Yanga kufanikiwa kumaliza kinara wa Kundi D kwa pointi 13 sawa na US Monastir ya Tunisia lakini Yanga ikikaa kileleni kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga.
Rivers ilimaliza ya pili kwenye Kundi B ikiwa na pointi 10 nyuma ya Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyojikusanyia pointi 13 baada ya mechi sita.
Kimataifa Yanga wapo tayari
Yanga wapo tayari
Read also